Washiriki wa mkutano wa kujadili utekelezaji wa mkakati wa kutokomeza mauaji ya wazee uliofanyika jijini Dodoma wakiwa katika majadiliano hayo
Wadau mbalimbali wanaoshughulika na masuala ya wazee nchini wamekutana kujadili hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa mkakati wa Kitaifa wa kutokomeza mauaji dhidi ya Wazee leo jijini Dodoma.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya - Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Sayi Magessa amesema tangu mkakati huo wa miaka 5 uzinduliwe mapema mwaka jana, idadi ya mauaji ya wazee imepungua kutoka 557 mwaka 2014 hadi wazee 74 mwaka 2019 na kueleza kuwa hadi mwaka huu idadi ya wanaouliwa kwa sababu mbalimbali ni chini ya wazee 10 kwa mwaka.
“Mkakati huu umesaidia sana kupunguza kutoka 557 mwaka 2014 hadi 74 mwaka 2019 lakini hadi sasa idadi inazidi kupungua hadi kufikia mmoja hadi tisa, kipindi kama hiki cha uchaguzi hali ilikuwa mbaya pia hata kwa walemavu kutokana na Imani potofu tu”
Ameongeza pia mkutano huu unalenga kuangalia mafanikio, changamoto na malengo zaidi ya baadaye ili kufanikisha kutokomeza kabisa mauaji ya wazee.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano huo, Kamishna wa Ustawi wa Jamii nchini Dkt. Naftali Ngóndi ametoa rai kwa vyombo vinavyohusika na upelelezi pamoja na hukumu kuhusu mauaji ya wazee kusaidia ili jamii itambue kuwa jambo hili ni kosa kwani wazee wana haki ya kuishi na kufurahia maisha.
“Mwisho wa siku tutatoka na maazimio ambayo kwa miaka iliyobaki historia ya kuua wazee iwe tumeisahau katika nchi yetu, nitoe rai kwa wenzetu wanaoshughulikia mifumo ya jinai kusaidia mchakato wa kupeleleza mauaji ya wazee pamoja na kuwahukumu wote wanaohusika, hii itatoa ujumbe kwa jamii kuwa hii siyo sahihi” alisema Ngóndi.
Naye Meneja wa Programu Haki kwa Wazee na ushirikiano wa Wadau kutoka Shirika la HelpAge International Joseph Mbasha amesema kwa ushirikiano na jitihada za wadau, nchi inakwenda vizuri katika kutokomeza mauaji ya wazee kwani takwimu zimepungua sana pamoja na kuwa barani Afrika nchi nyingi zilikumbwa na janga hilo kutokana na Imani potofu.
Mmoja wa Wazee walioshiriki mkutano huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa mashirika yanayotetea Wazee nchini Bi. Cotilda Isidory amesema tangu Serikali kupitia vyombo vyake mbalimbali iingilie kati suala la mauaji ya wazee, hivi sasa yamepungua kwa kiasi kikubwa kwani hapo kabla wameuawa wengi hali iliyokuwa inawatisha wazee hao.
Katika mkutano huo, washiriki walibainisha kuwa Serikali katika ngazi zote ikishirikiana na wadau ikiwemo vyombo vya Habari, kwa Pamoja walifanya jitihada kubwa kuhakikisha mauaji ya wazee yanakwisha.
Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ngóndi akitoa salamu kwa washiriki wa mkutano wa kujadili utekelezaji wa mkakati wa kutokomeza mauaji ya wazee uliofanyika jijini Dodoma. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango Sayi Magesa na kulia ni Mwakilishi kutoka TAMISEMI Mariam Mkumbwa.
Picha ya Pamoja ya washiriki wa mkutano wa kujadili utekelezaji wa mkakati wa kutokomeza mauaji ya wazee uliofanyika jijini Dodoma. Waliokaa kutoka kulia ni Mwenyekiti wa wazee Mkoa wa Shinyanga Mzee Sengerema, Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi, Mwenyekiti wa Mtandao wa mashirika yanayotetea wazee nchini Cotilda Isidory, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Sayi Magessa na mwakilishi kutoka Idara ya Operesheni na Mafunzo Jeshi la Polisi Boniphace Isaack.
Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii kutoka Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Mwanaisha Moyo akichangia jambo katika mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa mkakati wa kutokomeza mauaji ya wazee
Picha na WAMJW