MSABILA MALALE AZINDUA KAMPENI IBADAKULI, KIRUMBA NA MAYENGA WAMPIGIA DEBE

Wagombea ubunge viti maalum Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Santiel Kirumba (kushoto) na Lucy Mayenga (kulia) wakiwa kwenye uzinduzi wa mkutano wa kampeni mgombea udiwani kata ya Ibadakuli Jimbo la Shinyanga Mjini, Msabila Malale.

Na Mwandishi wetu, Shinyanga
ZIKIWA zimebaki siku takribani 37 kufikia Oktoba 28, 2020 kwa ajili ya kupiga kura kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani, mchaka mchaka wa kampeni kwa wagombea mbalimbali umzidi kuchanja mbuga, ambapo leo Septemba 21, mwaka huu ilikuwa zamu ya Mgombea udiwani wa Kata ya Ibadakuli katika Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CCM, Msabila Malale kuzindua kampeni zake na kunadi sera kwa wananchi.

Msabila amezindua kampeni zake kuomba ridhaa ya wananchi wa Kata ya Ibadakuli leo kwenye uwanja cha Shule ya Msingi Ibadakuli, huku akiwaomba wananchi kumwamini na kumchagua tena kwa mara ya pili. 

Amesema kuwa iwapo akipata ridhaa ya kuongoza tena kwa mara nyingine katika kata hiyo, atahakikisha anakamilisha miradi iliyobaki ikiwemo kupeleka maji katika kijiji cha Bugwandege, kwani katika awamu yake iliyopita amefikisha maji katika kijiji cha Uzogore ambapo kijiji hicho hakikuwahi kuwa na maji tangu Tanzania ilipopata uhuru mwaka 1961.

"Naombeni tena ridhaa yenu niwaletee maendeleo na kuendeleza pale tulipoishia, nawaahidi kwamba mkinipitisha tena nitasimamia kikamilifu ujenzi wa Stendi ya mabasi ya manispaa ya Shinyanga inayotarajiwa kujengwa katika kata hiyo," alisema.

Uzinduzi huo wa kampeni ulihudhuriwa na wagombea ubunge Viti Maalum mkoa wa Shinyanga kupitia CCM, Santiel Kirumba na Lucy Mayenga, ambao waliwasihi wananchi wa Ibadakuli kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi kwa sababu kinafanya kazi yake kikamilifu na kutekeleza ahadi zake.

Lucy Mayenga pia alimuombea kura kwa wananchi hao, Mgombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia chama hicho, Patrobas Katambi ili aweze kusimamia kazi za serikali na kuhakikisha kuwa analeta umeme wa REA sehemu za vijijini.

Mgombea udiwani kata ya Ibadakuli, Msabila Malale (wa kwanza kulia) Lucy Mayenga (wa pili kulia), mgombea udiwani viti maalum, Zuhura Waziri (katikati) na mgombea ubunge viti maalum mkoa wa shinyanga, Santiel Kirumba (kushoto) wakifuatilia mkutano huo wa kampeni




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464