MWALIMU AUAWA KWA KUPIGWA RISASI NYUMBANI KWAKE


MWALIMU wa Shule ya Sekondari Kihenya, wilayani Kasulu mkoani Kigoma, ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi akiwa nyumbani kwake.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, ACP James Manyama, alisema tukio hilo limetokea Septemba 6, majira ya saa tatu usiku, baada ya watu hao kuvamia nyumba ya mwalimu Fredrick Richard (30), aliyekuwa akiishi na mke na watoto wawili.
 
Alisema watu hao hawakuongea neno lolote baada ya kuingia ndani, walimpiga risasi mwalimu huyo na kuondoka bila kuchukua kitu chochote.
 
Jeshi hilo linamshikilia mtu mmoja akihusishwa na mauaji hayo baada ya polisi kuokota kofia katika eneo la tukio iliyosaidia kumpata mtuhumiwa huyo huku watuhumiwa wengine wakiendelea kutafutwa ili waunganishwe na mwenzao.
 
Kamanda alisema huenda tukio hilo ni la kulipa kisasi kwa kuwa wahalifu baada ya kutekeleza mauaji hawakuiba, hivyo kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.
 
“Nitoe wito kwa wananchi wa Kigoma waache kuchukua sheria mkononi kwa kuwa kitendo hicho cha mauaji ya mwalimu kinadumaza jitihada za kuinua kiwango cha elimu,” alisema.
 
Pia alisema kufuatia msako waliouendesha wamefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 21 na kuwakabidhi kwa Uhamiaji ili taratibu zingine ziendelee.
 
 Kamanda Manyama alisema hali ya ulinzi na usalama kwa Mkoa wa Kigoma kwa sasa ni shwari hivyo wananchi waishi kwa amani na wawe mstari wa mbele kusaidiana na jeshi hilo kutoa taarifa vinapotokea viashiria vya uhalifu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464