MWALIMU MKUU ANASWA TUHUMA ZA RUSHWA YA NGONO KWA MWANAFUNZI WAKE

MWALIMU mkuu wa shule ya msingi Nyeregete Wilayani Mbarali Mkoani Mbeya , Adelhard Mjingo (44) anashikiliwa na taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kosa la kutaka rushwa ya ngono kwa mwanafunzi wa darasa la saba mwenye umri wa miaka 14.


Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Mbeya Julieth Matechi amesema, ofisi yake ilipokea taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Nyeregete kuombwa rushwa ya ngono na mwalimu wake mkuu.

Matechi amesema, mwalimu huyo alifanya hivyo kwa ahadi ya kumsaidia katika mtihani wake wa darasa la saba huku akimtishia mwanafunzi huyo kuwa, endapo angemkatalia kufanya nae mapenzi angefanya kila liwezekanalo kuhakikisha anafeli mtihani.

Amesema, Takukuru baada ya kupata taarifa hiyo ilifuatilia na kujiridhisha na baadaye mtego ukawekwa jambo lililofanikisha kumkamata kwa mwalimu huyo septemba 23 mwaka huu, ndani ya nyumba ya kulala wageni (iitwayo Executive), iliyopo Rujewa akiwa na mwanafunzi wake kabla mtuhumiwa hajatekeleza dhamira yake uovu dhidi ya mwanafunzi huyo.

Hata hivyo Matechi amesema, siku ya tukio mwalimu huyo alikuwa ameaga shuleni kuwa anaenda kwenye semina ya chanjo Rujewa ambapo aliondoka na walimu wenzake.

Amesema, baada ya kufika kwenye semina alisaini na kuomba udhuru na kuelekea kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni, na wakati huo alikuwa amekwisha mwambia mwanafunzi wake arudi nyumbani kwa ajili ya kubadili nguo ili aende eneo la kibaoni na kumtuma mwendesha bodaboda aende kumchukua na kumpeleka eneo la tukio.

“Akiwa bado hajatimiza lengo lake ndipo makachero wa Takukuru walizokuwa wakifuatilia tukio hilo, wameingia ndani ya numba ya kulala wageni na kumuweka chini ya ulinzi mwalimu huyo,” amesema.

Matechi amesema, uchunguzi wa tuhuma hiyo unaendelea kwa mujibu wa sheria na baada ya kukamilika hatua zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani. Hata hivyo amesema, kukamatwa kwa mwalimu huyo ni matunda ya uanzishwaji wa klabu za wapinga rushwa mashuleni na vyuoni na mafunzo ya kampeni ya vunja ukimya kataa rushwa ya ngono ambayo imeendelea kuitoa kwa vijana ili kuwajengea ujasiri kukataa rushwa ya ngono kwa kutoa taarifa na kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya rushwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464