Mwanafunzi wa shule ya sekondari Kiagata, Mwita Juma (kulia) akishuka kwenye gari la polisi kwa ajili ya kusikiliza shauri linalomkabili la kumkata panga mwalimu wake.
Mwanafunzi Mwita Juma miaka 19 makazi wa kijiji cha Kyakoma kata ya Kiagata wilayani Butiama mkoani Mara amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wilaya ya Musoma akikabiliwa na kosa la kumjeruhi kwa panga Mwalimu wake Majogoro John kinyume na kifungu cha sheria namba 222 (a) cha kanuni ya adhabu kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.
Akisoma hati ya mashitaka wakili wa serikali Mwanadamizi Valence Mayenga mbele ya Hakimu Tumaini Marwa katika kesi namba 13 ya mwaka 2020 amesema mnamo tarehe 22 mwezi Septemba 2020 mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo akiwa eneo la shule ya Sekondari ya Kiagata kwa kumkata kwa panga Mwalimu Majogoro John pale ambapo mwalimu huyo alipo mwamuru akalete wazazi wake.
Mara baada ya mtuhumiwa huyo kusomewa shitaka, mtuhumiwa hakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na Hakimu Tumaini Marwa alisema uchunguzi wa kesi hiyo bado unaendelea na kuhairisha kesi hiyo hadi tarehe 12 Mwezi October 2020 ambapo kesi hiyo itakapo tajwa tena mahakamani hapo.
Hakimu Marwa amesema dhamana ya mshitakiwa ipo wazi na mshitakiwa anatakiwa kuwa na mdhamini mmoja ambapo masharti ya dhamana ni shilingi milioni 10, mali isiyo amishika iwe na hati ya umiliki na mdhamini ambatanishe na barua ya utambulisho kutoka makazi anayokaa mshitakiwa alikosa mdhamini na kupelekwa rumande hadi pale kesi hiyo itakapo tajwa tena.