Panga
Jeshi la polisi mkoani Mara linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha tatu Mwita Machamo,(17) katika shule ya sekondari ya Kiagata kwa kumkata na panga mwalimu wake Majogoro John, baada ya mwanafunzi huyo kushindwa kumpeleka mzazi wake shuleni kama alivyoagizwa na mwalimu.
Taarifa hiyo imetolewa leo Septemba 24, 2020, na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mara Daniel Shillah, na kusema kuwa tukio hilo lilitokea shuleni hapo majira ya asubuhi wakati mwalimu anakagua wanafunzi watoro, na ndipo mwanafunzi huyo alimgeukia mwalimu wake na kumkata mapanga.
"Baadhi ya wanafunzi waliwaleta wazazi wao, lakini huyu mwanafunzi kwa utovu wa nidhamu uliopindukia alikuja na upanga akiwa ameuficha kwenye nguo zake na mwalimu alipohoji kwanini hujaja na mzazi, mwanafunzi akachomoa upanga na kumshambulia mwalimu na akawatisha tisha wanafunzi wengine akapata nafasi ya kukimbia lakini wakamkata na tumemshikilia na atafikishwa mahakamani", amesema Kamanda Shillah.
Majogoro John ni mwalimu aliyejeruhiwa na mwanafunzi wake hapa anasimulia hali ilivyokuwa, "Nilipita darasani kuangalia watoro nikamuambia fuata mzazi tuje tuongee ili nijue shida nini yulke akatembea hatua kama tatu kwenda mlangoni akageuka alivyotoa upanga akageuka haraka akanikata begani akageuka tena ili anikate kichwani ndio nikaweka mkono wa kushoto akaiga panga nikaona tu mkono unaning'inia".
Kwa upande wake mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara Joachim Iyembe, amesema kuwa wamempokea mgonjwa huyo na kumpa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464