PROF. MSANJILA AELEZA ONGEZEKO LA SH BILIONI 528 MAKUSANYO SEKTA YA MADINI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila akizungumza na washiriki wa maonesho ya tatu ya teknolojia na uwekezaji kwenye sekta ya madini katika uwanja wa kituo cha uwekezaji Bombambili mjini Geita.

Leo Septemba 23, 2020 Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amefungua kongamano la biashara na uwekezaji katika Maonesho ya Tatu ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea katika Uwanja wa Kituo cha Uwekezaji wa Bomba Mbili Mjini Geita.

Kongamano hilo lilikutanisha wadau wa madini kwa lengo la kujadili na kujenga uelewa wa pamoja wa fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini ndani ya mkoa wa Geita.

Wadau walioshiriki katika kongamano hilo ni pamoja na wawakilishi kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zake, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Kampuni za Uchimbaji wa Madini, Wawakilishi kutoka Chama cha Wachimbaji wa Madini wa Mkoa wa Geita (GEREMA) Benki Mbalimbali na Taasisi nyingine za Serikali.

Kupitia hotuba yake Profesa Msanjila aliwataka wananchi wa mkoa wa Geita kuchangamkia fursa za uwekezaji kwenye Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na kutoa huduma mbalimbali kwenye kampuni zinazojihusisha na uchimbaji wa madini ikiwa ni pamoja na ulinzi na vyakula.

Akielezea mafanikio katika Wizara ya Madini, Profesa Msanjila alieleza kuwa ni pamoja na ukusanyaji wa maduhuli kutoka shilingi bilioni 160 hadi shilingi bilioni 528 ndani ya kipindi cha miaka mitano, ongezeko la kasi ya utoaji wa leseni za madini, kutengwa maeneo zaidi kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini.

Katika hatua nyingine Profesa Msanjila aliziomba taasisi za kifedha kutokusita kutoa mikopo kwa wachimbaji wa madini na wajasiriamali wanaotoa huduma kwenye kampuni za uchimbaji wa madini.

Aidha, Profesa Msanjila aliwataka wananchi kuzalisha bidhaa bora ili kupata soko la uhakika kwenye kampuni zinazochimba madini.

“Nia yetu kama Serikali ni kuhakikisha Sekta ya Madini inawezesha ukuaji wa sekta nyingine kama vile kilimo na uvuvi, tunatamani kuona hata madini yakiisha, kunakuwepo na ukuaji wa sekta nyingine zitakazowezesha uchumi wa nchi kupaa.

Aidha, Profesa Msanjila aliipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, Wizara ya Madini na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kwa maandalizi mazuri ya maonesho hayo.

Taasisi zilizopo chini ya Wizara zinazoshiriki katika maonesho hayo ni pamoja na Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Chuo cha Madini Dodoma (MRI), Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC), Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Mgodi wa STAMIGOLD. 




 
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464