JPM: SIKUTEGEMEA MAPOKEZI HAYA MWANZA, SASA NINA DENI


Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt John Pombe Magufuli akiwasalimia wananchi waliofurika katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza leo.

Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt John Pombe Magufuli, amesema kuwa hakutegemea kama angekutana na umati mkubwa wa watu uliojitokeza katika uwanja wa CCM Kirumba Mwanza kusikiliza sera zake, ambapo amejiona analo deni kubwa la kufanya kazi kwa wakazi wa Jiji hilo.

Magufuli ametoa kauli hiyo hii leo Septemba 7, 2020, na kuwaahidi wana Mwanza wanaokaa milimani kuwa, katika kipindi kijacho hakuna mwananchi yoyote atakayebomolewa nyumba yake na huduma zote zitawafuata huko huko waliko.

"Mapokezi niliyoyapata kuanzia jana katika Mkoa huu wa Mwanza sijawahi kuyaona, sikutegemea kama Uwanja huu wa Kirumba utajaaa, wakati wa mpira watu huwa wanakaa pembeni katikati wanachezea mpira, lakini leo hata pa kuchezea mpira watu wamejaa, pembeni wamejaa na nje wamejaa", amesema Dkt Magufuli.

Akizungumzia suala la nyumba za milimani kubomolewa, Dkt Magufuli amesema, "Mwanza imebadilika sana hata hizi nyumba huko juu hazikuwepo, na katika mipango ya baadaye tunarasimisha hizo nyumba zilizopo huko juu, hakuna mtu akayebomolewa nyumba yake kule juu, Serikali itapeleka huduma zake kule kule juu, kaaeni kwa raha kwanza milimani ndiko kwenye hewa nzuri ya kuvuta".


Sehemu ya Wananchi waliohudhuria Mkutano wa Kampeni za Urais za Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi CCM Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza leo tarehe 7 Septemba 2020






Credit (Picha): Malunde 1 Blog
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464