SERIKALI KUNUNUA PIKIPIKI 300 ZA MAOFISA AFYA WA KATA

 

PIKIPIKI 280 zimenunuliwa mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya maofisa afya mazingira nchini waliopo katika kata ili kufuatilia shughuli za kinga katika maeneo yao.

Mkakati huo wa kununua pikipiki pia unaendelea katika mwaka wa fedha 2020/2021, ambapo serikali imepanga kununua pikipiki 300 kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu shughuli za kinga katika maeneo mbalimbali nchini.
 

Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Leonard Subi alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Siku ya Mazingira Duniani iliyofanyika juzi.

Alisema mkakati ni kuhakikisha afya ya mazingira inafuatiliwa kwa karibu. Alisema pia katika kuweka mazingira wezeshaji ya kiutendaji, serikali pia imenunua magari saba maalumu kwa ajili ya kusaidia utuatiliaji wa masuala ya afya ya mazingira katika mikoa 17 na halmashauri 86 zilizopo pembezoni hapa nchini.

Dk Subi alisema pia magari mengine sita, yatanunuliwa katika mwaka huu wa fedha 2020/0221 ili kusaidia ufuatiliaji wa masuala ya afya katika maeneo mbalimbali nchini. Pia mikoa hiyo 17 na halmashauri 86 zimenunua vitendea kazi ambavyo ni kompyuta mpakato na printa kwa ajili ya kurahisisha kazi.

Serikali imepanga angalau kila mkoa uwe na gari moja na kila ofisa afya katika kata atakuwa na pikipiki kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao katika jamii.

Dk Subi alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa aliyotoa kwenye mkutano wa maofisa afya wa mikoa nchini mwaka 2018.

Mambo hayo yanafanyika ili kuimarisha utoaji wa huduma za afya mazingira, ambazo ni muhimu katika kulinda na kuimarisha afya ya jamii hususani katika kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza na ya milipuko.

Alisema uboreshaji wa vyoo na maji shuleni kutachochea ufaulu shuleni, kwani wa- nafunzi hasa mabinti watapata muda zaidi ya wa kukaa shuleni na kujifunza, badala ya kujifungia majumbani pindi wanapokuwa kwenye hedhi.

Pia walimu na watumishi wengine waliopo shuleni, watapata mazungira mazuri ya kazi kutokana na uwepo wa maji na miundmbo ya usafi ikiwemo sehemu maalumu za kunawa mikono.

Alisema mafanikio hayo, yamekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza kasi ya kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza yanayoenezwa kwa njia ya uchafu. 

CHANZO: HABARI LEO

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464