SERIKALI imeagiza watumishi wote wa umma waliotia nia kwenye vyama vya siasa na hawakuteuliwa kugombea, warudishwe kazini katika nafasi na vyeo vyao kuanzia leo na walipwe mshahara wa kuanzia mwezi huu.
Aidha, watumishi wa umma wameonywa kutokukuwa sehemu au chanzo cha vurugu wakati huu wa kampeni na uchaguzi.
Naibu Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais Menejimineti ya Utumishi wa Umma, Dk Francis Michael aliyasema hayo wakati wa kufungua kikao kazi cha siku mbili cha Wizara ya Maji na watendaji wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.
Alisema Agosti 26 mwaka huu, ofisi yake ilitoa waraka unaotengua uamuzi wa awali wa kuwataka watumishi wa umma waliokwenda kutia nia ya kugombea nafasi mbalimbali wakiwa wameomba ruhusa au wamekwenda kimyakimya, kuchukua likizo bila malipo.
"Watumishi wa umma wote sasa wanatakiwa kuripoti kazini na kurejea katika nafasi zao na vyeo vyao haraka sana kuanzia Septemba 1 mwaka huu," alisema Dk Michael na kuongeza:
"Kuna taarifa zilizokuwa zimezagaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa watumishi wa umma waliokwenda kutia nia hawatarudishwa kazini. Taarifa hizi sio sahihi, wale wote ambao hawakuteuliwa wanapaswa kurejea kazini kwani mtumishi wa umma kuwa mfuasi wa chama cha siasa au kushiriki siasa na kupiga kura ni haki yake" alisema.
Vyama vya siasa vimekamilisha taratibu za kuwachagua watakaopeperusha bendera zao (za vyama) katika nafasi ya urais, wabunge na udiwani kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.
Dk Michael alisema kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma na Kanuni za Uchaguzi, watumishi wa umma ambao hawataendelea na nafasi zao kwenye utumishi ni wale ambao wameteuliwa na vyama vyao kugombea.
Pia Dk Michael alimuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Maji na wakurugeni watendaji katika wizara hiyo, kuwaandika barua haraka za kuwarejesha watumishi wa umma ambao walikuwa likizo bila malipo kwa sababu ya kushiriki shughuli za siasa.Aliwaonya watumishi wa umma kutokuwa sehemu au chanzo cha vurugu wakati huu wa kampeni na uchaguzi.
Alisema ingawa mtumishi wa umma ana haki ya kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa na kushiriki shughuli za siasa kwenye vyama vyao, lakini ushiriki kwao usioneshe upendeleo katika utumishi wao.
Hata hivyo alisema watumishi wa umma wanapaswa kuzingatia masharti ya ushiriki wao katika masuala ya siasa, ambayo ni kutotoa siri za serikali na kutotumia rasilimali za umma.
Alisema wasaidizi wa viongozi wakiwemo mawaziri, hawaruhusiwi kushiriki na kufanya kazi zao endapo mkuu wake wa kazi atakuwa amegombea, na endapo atataka kushiriki, itabidi achukue likizo ya bila malipo na akitaka kurejea ataandika barua ya kurejea.
"Kushiriki kwa wasaidizi hao, au magari ya serikali kunaweza kumsababishia mgombea kuvuliwa ubunge endapo itabainika ushindi wake umechangiwa au kutokana na jitihada hizo na gari la serikali kutumika kwenye kampeni" alisema.
Dk Michael alisisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kuwa waadilifu kwa mujibu wa Kanuni za Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma kwa mwaka 2005, ikiwemo ya kuwa na matumizi sahihi ya madaraka, matumizi mazuri ya fedha na rasilimali za umma, matumizi ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia, kutopokea rushwa na kutotumia kwa mambo binafsi wakati wa muda wa mwajiri.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Evaristo Longopa alisema watumishi wa umma wana haki ya kuwa wanachama wa kikundi au chama cha siasa, isipokuwa kwa watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na wale wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Alisema watumishi wa umma wanakatazwa kutamka au kutoa matamko yanayoidhalilisha serikali kwenye kampeni na kutumia rasilimali za umma yakiwemo magari. Alisema mtumishi atakayebainika kufanya hivyo, atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja kufukuzwa kazi.
"Ukumbuke kwa kufanya hivyo, mtumishi utaingia matatani ikiwamo kufukuzwa kazi na pia hata huyo uliyemsaidia akishinda ushindi wake unaweza kutenguliwa" alisema.