TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Dodoma, imebaini kuwapo kwa baadhi ya walimu wanaochukua Sh 200 kutoka kwa wanafunzi wanaochelewa shuleni ili wasiadhibiwe.
Vitendo hivyo vya rushwa vimebainika katika Shule ya Msingi Mlimagate Wilaya ya Kongwa baada ya kupokea taarifa kwa simu kutoka kwa mzazi mmoja, kwamba walimu hupokea hongo ya Sh 200 hadi 500 kutoka kwa wafunzi watoro na waochelewa wasiadhibiwe. .
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo alitoa taarifa juu ya tukio hilo pamoja na mengine, ambayo taasisi yake imeyabaini na kuwashikilia baadhi ya watuhumiwa.
Kuhusu kudai rushwa kwa wanafunzi, taarifa ilisema katika ufuatiliaji wao wamebaini ni kweli baadhi ya walimu wanafanya hivyo suala linaloweza kuchochea vitendo vya utoro na hata kuharibu maadili ya wanafunzi hayo.
“Kwa kuwa pia ni wajibu wetu kuzuia vitendo vya rushwa ,tumeanza kushirikisha uongozi wa shule, Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa na wanafunzi ili kudhibiti vitendo hivyo visivyo vya maadili,” ilisema taarifah iyo.
Katika tukio lingine, Takukuru wilaya ya Kongwa imemkamata Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Karume iliyopo Kata ya Kibaigwa, Mwakangale Mwasikila (51) kwa kosa la kushawishi na kupokea rushwa ya Sh 55,000 ili atoe cheti cha kuhitimu darasa la saba kwa kijana aliyehitaji ili kuomba kujiunga mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Tukio lingine ni la Mwenyekiti wa Mtaa wa Tampoi katika Halmashauri ya Mji wa Kondoa , Abbas Said (50) anayeshikiliwa kwa kuomba rushwa ya Sh 12,000 kinyume cha sheria .
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464