Baadhi ya wahamiaji haramu waliokamatwa na Idara ya Uhamiaji mkoani Shinyanga wiki iliyopita katika Kata za Tinde, Didia na Itwangi wilayani Shinyanga wakiwa wameajiriwa kazi za kuchunga mifugo na baadhi ya wakazi wa kata hizo. (Picha na Suleiman Abeid)
Na Chibura Makorongo -Shinyanga
IDARA ya Uhamiaji Mkoani Shinyanga imewakamata jumla ya wahamiaji haramu 19 katika operesheni zake mbili za hivi karibuni, ambapo wahamiaji wapatao tisa walifikishwa katika Mahakama ya wilaya ya Kahama na kuhukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka miwili gerezani baada ya kukiri kuingia nchini kinyume cha sheria.
Naibu Kamishina wa Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga, Rashid Salum Magetta alisema watuhumiwa hao walikamatwa wiki iliyopita kufuatia opresheni maalumu ya kuwasaka wahamiaji haramu katika mkoa mzima wa Shinyanga wanaohisiwa kuingia nchini kwa njia za "panya" na kwenda kuishi vijijini.
Hata hivyo Naibu Kamishina Magetta alifafanua kwa kusema watuhumiwa watatu miongoni mwa tisa ndiyo waliopelekwa gerezani na kuanza kutumikia adhabu yao huku wengine sita wakisafirishwa na kurejeshwa nchini kwao Burundi baada ya kubainika umri wao ulikuwa chini ya miaka 18.
Pia Kamishina huyo alisema idara yake mwishoni mwa wiki iliyopita waliendesha Opresheni nyingine na kufanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu wengine wapatao 10 wakiwemo watoto saba ambao wote kwa pamoja wanatuhumiwa kuingia nchini kinyume cha sheria.
Waliokamatwa mwishoni mwa wiki wametajwa kuwa ni watu wazima wawili ambao ni Helesimana Dyson (18) na Kajana Simon (18) wengine ambao ni watoto Bukulu Ozia (17), Manilakuze Byatoli (17), Sengiyumwa Viane (16), Niyonzima Ponsian (17), Stephen Nongulu (14), Erick Niyogusenga (15) John Nyimbona (13) na Joachimu Thomas (14).
Magetta alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika msako maalumu uliofanyika kwa siku tatu mwishoni mwa wiki iliyopita katika kata za Tinde, Didia na Itwangi wilayani Shinyanga ambapo wengi wao walikuwa wameajiriwa kufanya kazi za kuchunga mifugo.
Baada ya kufanya mahojiano ya kina na watuhumiwa hao ilibainika wengi wao bado wana umri wa chini ya miaka 18 hivyo iliamriwa warejeshwe makao chini ya ulinzi wa watumishi wa Idara ya Uhamiaji ambapo walikabidhiwa katika mpaka wa Kabanga ili warejeshwe makwao.
“Naomba niwatahadharishe wananchi wetu na pia kutoa onyo kwa wale wote wenye mazoea ya kuwahifadhi wahamiaji haramu katika mkoa wetu waache mara moja tabia hiyo, maana tumebaini wapo watu wanaowapokea na kuwaajiri kazi za ufugaji ama kilimo.
“Kila mwananchi hapa nchini anapaswa kuheshimu sheria za nchi zilizopo ikiwemo za kutowapokea watu kutoka nchi nyingine bila ya kufuata utaratibu, lazima waelewe kufanya hivyo ni kosa kubwa, maana uwepo wa raia wa kigeni waliongia nchini kinyume cha sheria kunaweza kuwa chanzo cha vurugu na kusababisha amani tuliyonayo kutoweka,” alieleza Magetta.
Naibu Kamishina Magetta amewaomba wakazi wote wa Mkoa wa Shinyanga kuonesha uzalendo wao kwa kutoa taarifa katika vyombo husika inapotokea wamemuona mtu au watu wanaowatilia mashaka hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi nchini ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka.
Pia alisema ni vyema kila mwananchi anayetaka kuajiri mtu wa kumfanyia kazi mfano kilimo ama za kuchunga mifugo akawa makini na mtu anayemwajiri sambamba na kumuomba vitambulisho vinavyotambulika ikiwemo barua za wenyeviti wa Serikali za Mitaa.
“Ni vyema wananchi wetu wakaelewa kuwa kipindi hiki ni cha uchaguzi mkuu, watanzania tunapanga safu ya viongozi wetu watakaotuongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano, hivyo lazima tupate watanzania halisi, tusipokuwa makini tunaweza kujikuta tukiongozwa na watu wa mataifa mengine,” alieleza.