WATU watano wakiwamo viongozi wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanashikiliwa na Polisi mkoani Njombe kwa tuhuma za mauaji ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Vyuo Vikuu mkoani Iringa, Emmanuel Mlelwa.
Waliokamatwa ni Thadeus Mwanyika ambaye ni mgombea udiwani Kata ya Utalingolo (Chadema), George Sanga pia mgombea udiwani Kata ya Ramadhani (Chadema), Optatus Mkwera ambaye ni Katibu Mwenezi Kata ya Ramadhani (Chadema) na Godluck Mfuse ambaye ni dalali wa magari ya mizigo Njombe.
Aidha, gari la Sanga, mmoja kati ya watu wanaoshikiliwa na Polisi ambalo linadaiwa lilihusika kutekeleza mauaji hayo, Polisi imesema lilikutwa na mkanda wa kiunoni wa marehemu upekuzi ulipofanyika na wanalishikilia.
Tukio hilo limetoka mwezi sasa baada ya jingine kuripotiwa mwishoni mwa Agosti mwaka huu mkoani Songwe, likihusisha kifo cha Briton Mollel anayedaiwa kuwa kada wa CCM kikihusisha ugomvi kati ya wafuasi wa CCM na wa Chadema. Watu 16 walikamatwa na tayari wamefikishwa mahakamani.
Akizungumza nagazeti hili jana kuhusu kifo cha Mlelwa, Kamanda wa Polisi wa Njombe, Hamis Issah alisema Septemba 2, mwaka huu alipotea baada ya kutokuonekana kwenye kampeni kama ilivyotarajiwa na mchana taarifa ziliwafikia kuwa mwili umeonekana Kibena.
“Tulipofika kweli tuliukuta tukauchukua na kuuhifadhi Hospitali ya Kibena. Tarehe 24 mwezi huu ikaja taarifa kwamba kuna mtu haonekani, tukawahoji ndugu tarehe 26 na tulipokwenda nao hospitali wakathibitisha ni ndugu yao huyo Emmanuel Polycarp Mlelwa ambaye alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa,” alisema Issah.
Kamanda Issah alisema ndugu waliwaeleza kuwa Mlelwa alikuwa akiongeza nguvu kwenye kampeni,na baadhi ya watu walidai alikuwa akisimama jukwaani, watu wa vyama vingine wanahamia CCM kutokana na nguvu ya ushawishi aliyokuwa nayo.
Alisema siku ya tukio inadaiwa alizungumza na mtu aliyedaiwa kuwa ni mgombea udiwani wa Chadema (Mwanyika) akimjulisha kuwa waonane kwani anataka kujiunga na CCM.
“Usiku wakamwita sehemu inaitwa FM Njombe kuelekea Njombe Sekondari na huyo diwani baada ya kumkamata na kumhoji alidai kuwa walitekwa, lakini yeye yupo hai mwenzake amekufa na tulitumia sayansi kumbaini kuwa huenda ni mhusika kwa kuwa muda mfupi kabla ya kifo simu ilipozimwa, aliongea na Mwanyika na alikuwa naye,” alisema.
Akifafanua, alisema Mwanyika aliwataja wenzake aliyokuwa nao kuwa ni Sanga, mwenye gari lililowateka aina ya Toyota Gaia yenye namba za usajili T457DAB ambalo lilikutwa na mkanda uliothibitishwa na ndugu kuwa ni wa marehemu, Mkwera na Mfuse.
Kamanda alisema upelelezi unaendelea na huenda watu zaidi wakakamatwa kuhusika na tukio hilo, kwa kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa ni tukio la njama linalohusisha mtandao.
Aliwasihi wananchi wakiona au kuhisi kuna tukio lolote la uvunjifu waamani wakati huu wa kampeni, watoe taarifa polisi.
Agosti mwaka huu mkoani Songwe, watu 16 walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Songwe kwa tuhuma za mauaji ya anayedaiwa kuwa kada wa CCM, Mollel.
Mauaji hayo yalitokea baada ya kuzuka vurugu kati ya watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CCM na Chadema na kusababisha watu wengine wawili kujeruhiwa ambao Francis Simumba na Elisha Sifa.
Waliofikishwa mahakamani hapo ni Peter Charahani, Ijumeleghe Mwanjila , Elia Sichone, Charles Simkonda, Daudi Mwajunga, Wiliam Simkoko, Oscar Philip, Yohana Mkumbwa, Feston Kitta, Tonny Siwale, Ayubu Mwakasege, James Simkoko, Julius Wilson, Emmanuel Msinjili, Hidaya Mwangoka, na Jenifer Mwasenga.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Kassim Mkwawa, alidai watuhumiwa walitenda kosa hilo Agosti 25, mwaka huu katika eneo la Kata ya Mwakakati katika Mji wa Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464