WAFUGAJI KUNUFAIKA KWA KUPATIWA MAPORI YASIYOENDELEZWA KWA AJILI YA MALISHO




SERIKALI imesema imeanza kuweka utaratibu wa kugawa mapori yasiyoendelezwa kwa wafugaji ili wapate maeneo ya kulishia mifugo.
Pia, inaendelea kuwachimbia mabwawa ya kunyweshea maji mifugo hiyo ili kuondoa tatizo la ukosefu wa malisho na migogoro baina ya wakulima na wafugaji nchini.

Hayo yalibainishwa jana wilayani Misungwi mkoani Mwanza na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akiwaombea kura wagombea wa urais, ubunge na udiwani wa CCM.

Majaliwa alisema serikali inatambua umuhimu wa wafugaji nchini, ndio maana hata wizara iliyokuwa ikishughulika nao hivi sasa imekuwa wizara kamili inayojitegemea ya Mifugo na Uvuvi kutoka iliyokuwa Wizara ya Kilimo. Alisema lengo la hatua hiyo ni kuhakikisha wagufaji na mifugo, inakuwa na uangalizi nzuri zaidi.

Alisema hivi sasa serikali mimeanza kugawa mapori yasiyoendelezwa kwa wafugaji nchini, ikiwa ni njia mojawapo ya kutatua changamoto za wafugaji na kuondoa migogoro baina yao na wakulima. Alisema pamoja na kupewa mapori hayo, bado serikali itachimba mabwawa maalumu katika mapori hayo kwa ajili ya mifugo kupata eneo la kunywa maji.

“Tunafanya hivi kuondoa migogoro na sekta nyingine, maana kuwapa mapori ya kulishia mifugo bila kuwajenga mabwawa ya maji, bado wafugaji wataendelea kutoka nje na mifugo yao kutafuta maji, na inawezekana ikaleta matatizo hivyo tutawachimbia na mabwawa humo humo ili kusiwepo tena tatizo la maji,” alisema.

Pia alisema maabara na kliniki za mifugo, zitaanzishwa katika maeneo mengi nchini ili kudhibiti magonjwa ya mifugo na kutoa ruzuku za dawa zote za mifugo ili kuwapunguzia mzigo wafugaji.

Alisema serikali imeamua kufanya hivyo ili kuwepo na mifugo ya kutosha kwa sababu nchi inahitaji viwanda vya kuchakata mazao ya nyama. Alisema kama hakuna mipango thabiti ya kuhakikisha mifugo iko salama, viwanda hivyo havitakuwa na tija.

Akizungumzia jinsi serikali ilivyoboresha sekta ya uvuvi, Majaliwa alisema kodi mbali mbali za mifugo na zana za uvuvi, zimeondolewa ili kuwasaidia wafugaji hao kunufaika na kazi hiyo.

Kuhusu sekta ya kilimo, aliwataka wakulima wa pamba kuanza kujiandaa msimu huu.

“Wakulima wa pamba najua msimu uliopita hamkupata matokeo mazuri, kwa sababu mvua zilikuwa nyingi. Msimu huu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeshatangaza mwenendo wa mvua na kwamba anzeni kuandaa mashamba kwa sababu ni msimu nzuri kwa zao la pamba,” alisema Majaliwa.

Akizungumzia wakulima ambao hawajalipwa fedha zao za mauzo ya zao hilo, alisema serikali itahakikisha wale wote wanaodai wanalipwa na hakuna atakayedhulumiwa.

Awali akitoa shukrani zake kwa wananchi wa Jimbo la Misungwi, aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Charles Kitwanga aliomba radhi wananchi na wale wote aliowakosea, akisema hata yeye amewasamehe wote waliomkosea. Aliwataka wananchi kumuunga mkono mgombea ubunge, Alexander Mnyeti na wagombea wengine wote wa CCM.
                                    Chanzo.habarileo
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464