Mgombea Ubunge Vitimaalum mkoa wa Shinyanga kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Lucy Mayenga akiwa amepiga magoti mbele ya wananchi katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni kwa Jimbo la Ushetu.
Na Salvatory Ntandu, Ushetu
Wito umetolewa kwa Wanawake wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga kuwashawishi wanaume wao kushiriki katika kampeni na baadae kujitokeza kwa wingi katika zoezi la upigaji kura kuwachagua viongozi wanaowataka katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.
Ombi hilo limetolewa Jana na Mbunge wa Viti maalum wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Shinyanga, Dk Christina Mzava katika Uzinduzi wa Kampeni za Ubunge Jimbo la Ushetu uliofanyika katika Uwanja wa Magufuli katika Kata ya Bulungwa ulioenda sambamba na kunadi sera cha Chama hicho.
Dk Christina Mzava akiwa amepiga magoti mbele ya Wananchi kuomba ridhaa yao ya kukichagua chama cha CCM.
Alisema kuwa Wanawake wanaweza kuwashawishi wanaume zao kwa kuwaeleza faida za kuhudhuria katika mikutano ya kampeni ili kusikiliza sera zilizo kwa Wagombea wa CCM wa gazi zote ikiwemo ya Urais kwa kumchagua Dk John Pombe Magufuli,Mbunge Elias Kwandikwa na Madiwani wote wa chama hicho.
“Wanawake sisi ni jeshi kubwa tunao uwezo wa kuwashawishi kwa kila mbinu wanaume wate wakapige kura za kuichagua CCM ili iendelee kuwaletea maendeleo,kila mtu anajua kazi zilizotekelezwa na serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk John Pombe Magufuli,”alisema Dk Mzava.
Alifafanua kuwa katika sekta ya afya Serikali inayoongozwa na CCM imeboresha upatikanaji wa huduma ikiwemo dawa na vifaa tiba sambamba na ujenzi wa Hospitali,Vituo vya afya na Zahanati kwa Kila Kijiji ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho ya Mwaka 2010-2015 ambayo imetekelezwa kikamilifu.
Kwa Upande wake Lucy Mayenga Mgombea Ubunge viti maalum mkoa wa Shinyanga kupitia (CCM) alisema kuwa Wanawake wanapaswa kuwachagua wagombea wote wa Chama hicho ili waende kuiunda serikali kwa kipindi kingine cha miaka mitano wakiongozwa na Jemedari Rais Dk John Pombe Magufuli.
“Najua watakuja wagombea wa vyama vingine hapa hebu pimeni sera za na ilani zao ikiwekana wapuuzeni, shida yao ni kulalamika tu na kufanya kampeni za matusi na zenye kuhamasisha chuki ili kuvuruga amani ya taifa letu ambayo ni tunu tuliyoachiwa na waasisi wa Taifa hili,”alisema Mayengo.
Nae Santiel Kirumba Mgombea Ubunge wa Viti maalum kupitia CCM mkoa wa Shinyanga aliwataka wananchi kuendelea kukiunga mkono chama hicho kwani kimeweza kutekeleza ahadi zake mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumtua mama ndoo maji, upatikanaji wa huduma ya Nishati ya Umeme vijijini na ujenzi wa barabara.
“Katika Jimbo hili zaidi ya bilioni 2 zimetolewa na serikali ya inayosimamiwa na CCM katika Ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Ushetu ili kuwapunguzia adha wakazi wa jimbo hili hususani akinamama wajawazito kwenda kahama umbali wa kilomita 50 kufuata matibabu ambapo kwasasa wameanza kupatiwa matibabu,”alisema Kirumba.
Awali akiwatambulisha Wagombea hao Ubunge wa Viti maalum (CCM) wa Mkoa huo, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa aliwataka kuhakisha wanakwenda kwa wapiga kura kuomba kuwashawishi kumpigia kura Rais,Wabunge na Madiwani ili chama hicho kiweze kupata ridhaa kuongoza kwa kindi cha miaka mitano ijayo.
Mgombea Ubunge Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Dk Christina Mzava akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni kwa Jimbo la Ushetu. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa.
Mgombea Ubunge Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Lucy Mayenga akiomba kura kwa wananchi wa jimbo la Ushetu. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa.
Mgombea Ubunge Viti maalum mkoa wa Shinyanga, Santilel Kirumba akizungumza na Wananchi katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni jimbo la Ushetu ili kuomba ridhaa yao kukichagua chama hicho. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa.