Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Kessy Maduka (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Dodoma, Iringa, Singida na Shinyanga wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili kuhusu utekelezaji wa kipindi cha pili awamu ya tatu (PSSN II) unaotekelezwa na TASAF. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga.
Na Shinyanga Press Club Blog–Dodoma
WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuwa sehemu muhimu ya kufanikisha utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini kipindi cha pili awamu ya tatu (PSSN II) unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ili kuhamasisha jamii na kuondoa uzushi juu ya mpango huo.
Hayo yameelezwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Kessy Maduka wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili kilichoanza Septemba 7 hadi 8, 2020 cha kujenga uelewa kwa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Iringa na Singida kuhusu utekelezaji wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya Tasaf (PSSN II).
Maduka alisema kuwa wanahabari wana wajibu wa kuwaelimisha wananchi wa kipato cha chini nini maana ya mfuko wa maendeleo ya jamii na mpango wa kunusuru kaya maskini kwa ujumla wake ili kufanikisha kuupiga vita umaskini na kuendeleza pato la kitaifa kwa kufikisha ujumbe na taarifa sahihi kwa walengwa wa mfuko huo.
“Wanahabari mtumie taaluma yenu juu ya mafanikio makubwa yaliyofikiwa kupitia mpango wa TASAF katika sekta mbalimbali nchini, pia mtumie fursa hiyo kujifunza na kuandika mafanikio yaliyofikiwa na walengwa ili yasaidie kubadilisha mtazamo wa wengi na kufuta upotoshaji unaofanywa kuhusu mpango huu.
“Ushiriki wenu katika kupiga vita umaskini ni kwa kutumia nafasi zenu kuandika na kutangaza habari zinazoonyesha matokeo chanya yanayotokana na utashi wa walengwa kujiondoa kwenye hali duni kwa kutumia ruzuku, elimu na ujuzi wanaoupata kupitia TASAF,” alisema.
Kutoka na utekelezaji wa TASAF kipindi cha pili awamu ya tatu kuchelewa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 mwanzoni mwa mwezi wa tatu mara baada tu ya mpango huo kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli mnamo Februari, mwaka huu, Katibu Tawala Maduka ameiomba TASAF kuwaomba wadau wa maendelo walio sehemu ya ufadhili kuongeza muda wa utekelezaji hadi mwaka 2025 badala ya 2023.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga alisema katika awamu hii ya tatu jumla ya kaya karibu takriban 800, 000 zinatarajiwa kunufaika baada ya uhakiki kufanyika, huku kaya 1,320 zikiomba kwa hiari kuondolewa baada ya kupiga hatua na kujikwamua kwenye umaskini.
Mwamanga pia alieleza kuwa baada ya mchakato wa uchaguzi mkuu kukamilika Oktoba 28, 2020, wataendelea kuelimisha wadau wengine wakiwemo watendaji wa halmashauri na wabunge ili kusiwe na sintofahamu wakati wa utekelezaji na kila mmoja atomize wajibu wake.
Gharama za utekelezaji wa mpango katika kipindi cha pili awamu ya tatu ya TASAF ni Sh Trilioni 2.05 ambazo ni wastani wa asilimia 0.5 ya pato la taifa, huku asilimia 20 ya kaya zikitarajiwa kuhitimu kutoka kwenye mpango baada ya kuwa na hali nzuri.
Akizungumzia kuhusu kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF kinachotarajiwa kuanza kutekelezwa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu, Mkurugenzi wa Huduma za Jamii Tasaf, Amadeus Kamagenge alisema kuwa kipindi hiki ni cha miaka minne (2020-2023) na mradi utapanuliwa na kutekelezwa katika asilimia 30 ya vijiji/shehia ambazo hazikufikiwa kipindi cha kwanza na kuandikisha kaya maskini sana kwenye maeneo hayo ambazo hazikuandikishwa kwa sababu mbalimbali.
Hivyo, utekelezaji wake utafanyika kwenye mamlaka za maeneo 187 (halmashauri 185 za Tanzania Bara na Unguja na Pemba, Zanzibar), ambapo kiwango cha chini kwa mwezi kwa mnufaika kitakuwa Sh 12,000 na kiwango cha juu kwa mwezi Sh 55,000.
Katika hatua nyingine, Kamagenge alieleza kuwa katika kipindi hiki kaya za walengwa zitalipwa ruzuku zao kwa njia ya kielektroniki, ambapo mwakilishi wa kaya atapokea ruzuku kwenye akaunti yake ya benki au ya simu na usajili utafanyika kwa kutumia vitambulisho ama namba za NIDA kuwatambua walengwa ili kuwalipa.
Katika kikao kazi hicho cha siku mbili kilichomalizika leo Septemba 8, 2020 jijini Dodoma, wanahabari hao walipata fursa ya kutembelea kaya zinazonufaika na mpango huo katika Kata za Nara na Hombolo mkoani humo kujionea namna zilivyopiga hatua na changamoto wanazokabiliwa nazo.
Serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mwaka 2000 kwa madhumuni ya kusaidiana na vyombo vingine vya serikali kupunguza umaskini, ambapo mfuko huo umekuwa ukitekeleza miradi mbalimbali katika ngazi ya jamii kwa lengo la kutoa huduma za jamii katika sekta zote kwa kuzingatia mahitaji halisi au kero za wananchi. Hadi sasa TASAF imetekelezwa katika awamu tatu.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga akizungumza wakati wa kikao hicho
Waandishi wa habari wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa na TASAF Katika kikao hicho
Mmoja wa wanufaika wa TASAF, Janeth Dede mkazi wa Mtaa wa Bwawani B Kata ya Hombolo jijini Dodoma akichoma vyungu kwa ajili ya kuwauzia wateja mbalimbali.
Juu ni nyumba mpya ya mmoja wa wanufaika wa Tasaf kata ya Nara jijini Dodoma aliyoijenga baada ya kunufaika na mpango wa kunusuru kaya maskini, chini ni nyumba ya zamani aliyokuwa akiishi.
Mnufaika wa mpango wa kunusuru Kaya Maskini katika mtaa wa Bwawani B, Eliza Mjega akihojiwa na waandishi wa habari waliofika kujionea baadhi ya hatua alizopiga kutokana na manufaa anayoyapata kwenye mpango huo.
Eliza Mjega na mmewe,Elisha Ndagabwene wakionyesha nyumba wanayoijenga ambayo ni matunda ya hatua walizopiga kutokana na mpango wa kunusuru kaya maskini.
Mnufaika wa Mpango wa Kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na TASAF, Marry Makago ambaye ni mlemavu mkazi wa Kata ya Hombolo jijini Dodoma akiwaeleza waandishi wa habari na maofisa wa TASAF namna anavyofaidika na mpango huo.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano TASAF, Zuhura Mdungi (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa mnufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini, Marry Makago
Muonekano wa nyumba anayoijenga mnufaika huyo (Marry Makago) kutokana na mafanikio anayoyapata kupitia Mpango wa kunusuru kaya maskini
Muonekano wa ukuta na nyumba anayoitumia kwa sasa
Mnufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini, Marry Makago (aliyeshikilia kalenda) akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari waliomtembelea nyumbani kwake Hombolo jijini Dodoma
Mnufaika wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini kutoka kijiji cha Bwawani B kata ya Hombolo mkoani Dodoma, Doris Chiteto akizungumza na waandishi wa habari waliofika nyumbani kwake kujionea namna alivyonufaika na mpango huo
Doris Chiteto akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari na maofisa wa TASAF waliomtembelea nyumbani kwake
Picha zote na Shinyanga Press Club Blog