Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Biswalo Mganga amewaachia huru washtakiwa 57, wakiwepo wanaume 47 na wanawake 10
waliokuwa wanakabiliwa na kesi mbalimbali ambao waliokuwa wamewekwa
katika gereza la Shinyanga.
Biswalo ameendesha zoezi
hilo wakati alipotembelea gereza la Shinyanga akiwa ameongozana na Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju pamoja na
viongozi mbalimbali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Wizara ya
Katiba na Sheria.
Akizungumza katika tukio hilo Bw. Amon Mpanju
amesema wametembelea gereza la Shinyanga ikiwa ni sehemu kuhakikisha mfumo wa
upatikanaji haki ili kwa pamoja kuweza kuwasikiliza na kufahamu
changamoto zilizoko kwenye magereza na kuzitafutia suluhisho.
Akizungumza
wakati akiwaachia huru mahabusu hao Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Biswalo
Mganga amewataka mahabusu hao waliochiwa huru kuhakikisha hawarudii
makosa waliyoyafanya kwa kuwa anahitaji nchi yenye amani huku akiwaeleza wazi kuwa yeyote kati yao ambae anajua hawezi kwenda kutulia na kuwa
raia mwema abaki gerezani.
Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba
na Sheria Bw. Amon Mpanju amewasihi mahabusu hao walioachiwa huru
wakirudi uraiani kwenda kuwa raia wema na wale waliobakia kukaa kwa
amani na kuwasikiliza walezi wao gerezani huku wakifundishana wao kwa
wao kutenda mema.
Awali kabla ya kuanza ziara ya kutembelea gereza
hilo la Shinyanga wajumbe walipata nafasi ya kumtembelea Mkuu wa Mkoa
wa Shinyanga Bi. Zainabu Telack na kuzungumza nae juu ya ziara hiyo
ambapo amepongeza juu ya hatua hiyo na kueleza kuwa ziara kama hizo
zitasaidia kutatua changamoto mbalimbali za magerezani.
Wakati wa
ziara hiyo ya kutembelea magereza wajumbe wamechangia kiasi cha shilingi
laki tatu (300,000/=)ambazo zimetolewa kwa lengo la kuliwezesha gereza
hilo kununua cherehani, sabuni na ving’amuzi kufuatia ombi la wafungwa
hao.
Chanzo (WWW.NPS.GO.TZ )