Na Damian Masyenene – Shinyanga
SAKATA la wagombea ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini, Patobass Katambi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Salome Makamba wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limeendelea kuchukua sura nyingine baada ya hii leo, Katambi kumtaka mpinzani wake huyo ajitokeze hadharani aombe radhi kabla hajamchukulia hatua zaidi za kisheria kwa kumdhalilisha na kudhalilisha wanawake.
Akizungumza leo Oktoba 16, 2020 na Waandishi wa habari mjini Shinyanga, Katambi amesema kuwa Salome amekuwa akizusha uongo na upotoshaji dhidi yake ili kutafuta kura za huruma kwa wanawake.
Mvutano baina ya wawili hao ambao ni washindani wa karibu kwenye mbio za ubunge wa jimbo la Shinyanga Mjini ulianza Oktoba 7, mwaka huu pale ambapo Katambi alipowasilisha malalamiko yake kwenye kamati ya maadili ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini akilalamikia ukiukwaji wa maadili unaoweza kusababisha vurugu au uvunjifu wa amani unaofanywa na Salome Makamba.
Katika barua hiyo ya Oktoba 7, 2020 Katambi alinukuliwa akisema kuwa mpinzani wake alitunga uongo na kuzusha ili apate kura za huruma na kumjengea chuki kwa wananchi akitangaza kusema kwamba katambi alisema "Salome asichaguliwe kwa kuwa ni mwanamke na akiwa hedhi hatafanya kazi".
Hata hivyo shauri hilo lilitolewa uamuzi Oktoba 13, 2020 na kamati ya maadili ambayo ilikutana Oktoba 10, mwaka huu ambayo ilimuita Salome Makamba ambaye alishindwa kutoa vielelezo mbele ya kamati, hivyo kamati ikaazimia mlalamikiwa apewe karipio kali na endapo hali hiyo itajirudia hatua kali zaidi zitachukuliwa dhidi yake.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari leo mjini Shinyanga juu ya uzushi wa mpinzani wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kwa tiketi ya CCM, Patrobas Katambi alimtaka Salome Makamba ajitokeze aombe radhi kwa wanawake baada ya kuwadhalilisha, pia aombe radhi kwa viongozi wa dini na wanasheria.
"Hii ni kashfa, alidhani jambo hili litampa nguvu na sifa za kutafuta kura lakini amejiaibisha, Mimi kama mkristu namsamehe lakini msamaha wangu ni mpaka ajitokeze hadharani awaombe radhi wanawake, asipofanya hivyo nitaenda mbele zaidi na kuchukua hatua za kufungua shauri lingine la kashfa na kuchafuliwa (Defamation) ili alipe fidia......siwezi kukubali mtu dhaifu na mchanga anidhalilishe na kunichafua," amesema Katambi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Shumbuo Yusuph amelaani kitendo cha mgombea wa Chadema (Salome Makamba) kuzusha uongo dhidi ya wanawake, ambapo amewaomba wanawake wa Shinyanga kumpuuza na kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani ndicho chenye sera za uhakika.
Naye Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini, Geoffrey Mwangulumbi amesema kuwa maaamuzi yaliyotolewa na kamati ya maadili ni sahihi na kuwataka ambao hawajaridhishwa na maamuzi hayo kuchukua hatua zaidi kwa kuwasilisha malalamiko yao kamati ya maadili kitaifa.
Hata hivyo, akizungumzia Sakata hilo, Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini Salome Makamba (CHADEMA) amesema
anaheshimu maamuzi ya kamati ya maadili huku akibainisha kuwa hajaridhika na
maamuzi hayo ya kamati ya maadili.
“Mimi ninaheshimu
maamuzi ya kamati ya maadili lakini naamini hawakunitendea haki kwa sababu
wanataka ushahidi wanaoutaka wao,nimepeleka kwenye kamati ya maadili watu wa
kuthitisha jambo hilo lakini wao wakakataa kuwasikiliza hao watu wakasema
hawana muda na kwamba hawajajiandaa kwa ajili ya kusikiliza mashahidi",amesema Makamba.
“Kwa hiyo
naheshimu maamuzi yao na tuendelee na kampeni na kuhusu kauli ya kudhalilisha
wanawake, Wapiga kura walimsikia alichosema Katambi, wao ndiyo wataaamua Tarehe
28,2020 kuwa nani anadhalilisha wanawake”,ameongeza Makamba.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kwa tiketi ya CCM, Patrobas Katambi akizungumza na waandishi wa habari leo
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kwa tiketi ya CCM, Patrobas Katambi akizungumza na waandishi wa habari
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Shumbuo Yusuph akitoa tamko la kulaani ya kauli ya Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini, Kupitia CHADEMA, Salome Makamba ya kudhalilisha wanawake
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Shinyanga Mjini, Geoffrey Mwangulumbi akizungumza na waandishi wa habari leo
Mgombea Ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CHADEMA, Salome Makamba akizungumza katika moja ya mikutano yake ya Kampeni.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464