AHMED KUMALIZA TATIZO LA MAJI SOLWA KUUNGANISHA VIJIJI VYOTE

 


                                                                         


Mgombea Ubunge wa Jimbo la Solwa Ahmed Salum akizungumza na wakazi wa Kata ya Didia Halmashauri ya Shinyanga wakati akifunga kampeni za uchaguzi.

Na Stella Herman Shinyanga Press Club Blog

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Solwa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM)Ahmed Salum,amesema iwapo  wakazi wa jimbo hilo watampa tena ridhaa ya kuendelea kuwa mbunge wao atahakikisha ifikapo mwaka 2022 kila kijiji kinakuwa na maji ya ziwa Victoria.

Hayo ameyasema leo wakati akifunga kampeni zake katika Kata ya Didia na kueleza kuwa amepambana kuhakikisha maji ya ziwa Victoria yanafika katika jimbo hilo jambo ambalo limefanikiwa na kilichobaki ni kuyafikisha vijiji vyote ili kuwaondolea kero wananchi ya kufuata maji umbali mrefu.

Ahmed amesema vijiji vyote 126 vitapata maji ya ziwa Victoria na kueleza kuwa huo ni mradi mkubwa unatumia fedha nyingi na unahitaji mtu makini atakaye weza kufuatili na kuhakikisha kero ya maji inabaki kuwa historia katika jimbo hilo ndani ya miaka michache ijayo.

Mbali na kukabiliana na changamoto ya maji pia ameahidi kushirikiana na serikali inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi kujenga kituo cha afya katika kata ya Lyabukande na kata ya Didia ambavyo vitasaidia kusogeza huduma karibu kwa wananchi.

Akizungumzia suala la miundombinu ya barabara amesema hakuna jimbo Tanzania lililopata barabara zenye kilomita 250 na kueleza kuwa inatokana na kuwa na mbunge asiye mbabaishaji anayejali kero za wananchi wake.

''  ili niweze kukamilisha mipango ya maendeleo niliyoianzisha ambayo bado haijakamilika naomba tena ridhaa yenu nifanye mabadiliko makubwa,barabara hii ya Didia na maeneo ya Kata zingine yote yatawekewa lami na tutapata wafanyabiashara wengi kutoka nchi jirani kuja kununua mazao katika kata hii "amesema Salum

Ameongeza kuwa mafanikio ni makubwa yaliyopatikana licha ya baadhi ya watu wanadai hakuna kilichofanyika,ambapo amewataka wananchi kuwapuuza kwani kazi yao ni kupinga maendeleo na kuwaomba kumchagua yeye kuwa mbunge wao,Richard Masele kuwa diwani wa Didia na kumpa kura za kishindo kesho Octoba 28 John Pombe Magufuli.

Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa kampeni

Mkutano wa kampeni unaendelea

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464