Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha (aliyevaa miwani) akipokea viti na meza kwa niaba ya Shule ya Sekondari Kitwana vilivyotolewa leo na Benki ya CRDB. Kushoto ni Meneja Biashara wa benki hiyo Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana
Na Shinyanga Press Club Blog
Benki ya CRDB kanda ya magharibi imetoa msaada wa viti na meza 88 katika shule ya Sekondari Kitwana Wilayani Kahama mkoani Shinyanga ikiwa ni muendelezo wa kusherehekea wiki ya huduma kwa wateja iliyoanza Jumatatu Octoba 5 mwaka huu.
Akipokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Annamringi Macha ameishukuru benki ya CRDB kwa kujitoa mara kwa mara kuchangia miradi ya maendeleo na kuziomba taasisi zingine kuiga mfano huo.
Macha ameongeza kuwa msaada huo wa viti na meza umepunguza kwa kiasi kikubwa kero iliyokuwepo katika shule ya Sekondari Kitwana licha ya kwamba mwakani halmashauri ya mji wa kahama ina mzigo mkubwa kutokana na wanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza kuwa wengi kuliko mwaka huu.
Kwa upande wake Meneja Biashara Benki ya CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana amesema kuwa msaada huo wa viti na meza umegharimu Shilingi milioni saba na kwamba Benki ya CRDB itaendelea kutoa misaada ya kijamii kupitia asilimia moja ya Faida wanayoitenga kila mwaka.
Sambamba na hayo Wagana ametoa wito kwa wadau na wananchi mbalimbali kuitembelea benki ya CRDB ili kujifunza mengi na kufungua Akaunti mbalimbali kupitia wiki ya huduma kwa wateja.
Naye Meneja wa CRDB Tawi la Kahama, Evod Kereti amewaasa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitwana kuwa kuna akaunti maalumu ya wanafunzi wa shule ya Sekondari ambayo kufungua ni bure na kwamba wakawaambie wazazi wao ili waweze kuwafungulia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Kitwana, Flora Cleopa Mwanri amewaomba wadau wa elimu kupitia Ofisi ya mkuu wa wilaya kusaidia upatikanaji wa Bweni la wasichana ili kuwaepusha mabinti na vishawishi vya ngono pamoja na kuwafanya wazingatie masomo.
Awali akisoma risala, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kitwana, Basil Kijazi ameishukuru benki ya CRDB kwa msaada huo na kuongeza kuwa kwa sasa kinachowakabili ni thamani za walimu kwani walimu wanatumia viti na meza za wanafunzi.
Benki ya CRDB imeendelea kusaidia misaada mbalimbali ya kijamii ikewemo Afya na Elimu kupitia asilimia moja ya Faida wanayopata kila mwaka katika matawi yake yote nchini.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitwana wilayani Kahama wakifurahi baada ya kupokea msaada wa meza na viti 88 kutoka benki ya CRDB Kanda ya Magharibi
Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Anamringi Macha (katikati) akiwa amekalia sehemu ya msaada wa meza na viti vilivyotolewa leo na Benki ya CRDB katika shule ya Sekondari Kitwana.