Jumanne Sagini akinadi sera na kuomba kura kwa wananchi wa Kijiji cha Bumangi wilayani Serengeti
Na Mwandishi wetu, Serengeti
Mgombea Ubunge Jimbo la Butiama mkoani Mara kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jumanne Sagini amesema kuwa awamu iliyopita wapinzani waliomba apatikane kiongozi atakayetumia muda mwingi kutatua kero za wananchi, ambapo Mwenyezi Mungu alijibu ombi lao kwa kumleta Dk. John Magufuli.
Akizungumza kwenye mkutano wa Kampeni uliofanyika mapema hii leo kijiji cha Bumangi Kata ya Muriaza, amesema kuwa Mungu alisikia kilio chao baada ya uchaguzi mkuu wananchi wakamchagua Rais Dk. John Magufuli ambaye alifanya mara mia ya walivyohitaji kwani ni kiongozi pekee aliyefaulu kudhibiti ufisadi na kuleta heshima serikalini.
"Ndugu zangu nawaombeni mumchague Rais wetu Magufuli kwani toka aingie madarakani amekuwa humu nchini akifuatilia utekelezaji na kero za wananchi na wala hajawahi kusafiri kwenda mataifa ya Ulaya," amesema Sagini.
Sagini ameeleza kuwa JPM aliteua mabalozi ambao wanafuatilia kwa umakini mambo ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na kutafuta wawekezaji na kushughulikia mambo ya kiserikali katika nchi wanazoiwakilisha Tanzania.
Aidha amewaomba wananchi ifikapo Oktoba 28, mwaka huu kuipigia kura CCM kuanzia nafasi za udiwani, ubunge na Rais kwa maendeleo ya Taifa.
Wananchi wa kijiji cha Bumangi kata ya Muriaza wilayani Serengeti mkoa wa Mara wakifuatilia mkutano wa kampeni wa Mgombea Ubunge wa Jimbo la Serengeti kwa tiketi ya CCM, Jumanne Sagini Oktoba 24, 2020.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464