Kaimu mwenyekiti wa amani mkoa wa Shinyanga Shekh Khalfani Ally, akizungumza na vyombo vya habari kutoa tamko la kamati hiyo kuelekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu.
Na Marco Maduhu- Shinyanga
Kamati ya Amani Mkoa wa Shinyanga imewataka Watanzania kutokubali kutumiwa na wanasiasa siku ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu ambao utafanyika Oktoba 28 mwaka huu, kutofanya fujo za aina zozote ambazo zitavuruga amani ya nchi.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Shekh Khalfan Ally, amebainisha hayo leo wakati akisoma tamko la viongozi wa dini mkoani humo, kuwa kumekuwapo na viashiria kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, kuanza kuhamasisha wananchi kufanya fujo siku hiyo ya uchaguzi.
Amesema Watanzania wanapaswa kuilinda amani ya nchi ambayo inatamaniwa na baadhi ya mataifa kuvurugika, bali wakatae kushawishiwa na baadhi ya wanasiasa kufanya fujo kwenye uchaguzi mkuu, ili kupeuka uvunjifu huo wa amani.
“Kamati ya amani mkoani Shinyanga inawataka watanzania kutokubali kutumiwa na wanasiasa kuvuruga amani ya nchi kwenye uchaguzi mkuu, bali siku hiyo wakimaliza kupiga kura warudi majumbani mwao kusubili matokeo na wasifanye maandamano ya aina yoyote ile,” amesema Ally.
“Uvunjifu wa amani ukitokea waathirika wakubwa ni watoto, akina mama, wazee na watu wenye mahitaji maalum, pamoja na uchumi wa nchi kuyumba, sababu hapatakuwa na shughuli zozote zile za maendeleo,” ameongeza.
Katika hatua nyingine kamati hiyo ya amani imewataka baadhi ya viongozi wa dini ambao wanahamasisha vijana kujitokeza kukaa barabarani na kwenye vituo vya kupigia kura, hali ambayo ni viashiria vya kufanya vurugu za uvunjifu wa amani, waachane na tabia hiyo ambayo ni kinyume na misingi ya dini.
Naye Mjumbe wa Kamati hiyo, John Kilinda ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la waadventista Wasabato Shinyanga Mjini, alisema mfumo wa vyama vingi uliwekwa kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya nchi, lakini baadhi ya vyama vya siasa vimeanza kuutumia vibaya.
Aidha amewataka viongozi wa vyama vya siasa, wazitumie siku hizi zilizosalia kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, wanadi sera zao kwa wananchi ili wapate kukubalika na kuchaguliwa, na siyo kutaka kutumia nguvu kupata madaraka, na kuhamasisha wananchi kuingia barabarani kufanya maandamano ambayo yatagharimu maisha yao.
Viongozi wa kamati ya amani mkoani Shinyanga wakiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Shekh Soud Kategile akizungumza kwenye mkutano huo.
Mchungaji wa kanisa la Waadventista Wasabato Shinyanga mjini John Kilinda, akizungumza kwenye mkutano huo.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano huo na kamati ya amani mkoani Shinyanga,