Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dk. Wilson Charles
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema kuwa kampuni ya Ren-Form CC ya Afrika Kusini ndiyo iliyoshinda zabuni ya kuchapisha karatasi za kupigia kura.
Aidha, NEC imesema kulikuwa na ushindani katika mchakato wa kupata mzabuni na makampuni matatu yaliomba ambayo mengine ni Ellams Products Limited ya Kenya na Al Ghurair Printing and Publication LLC ya Dubai.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na umma na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk. Wilson Charles, madai kuwa kampuni ya Jamana Printers ilipewa kazi hiyo hayana ukweli.
Alisema mchakato wote ulizingatia sheria na tangazo la fursa za zabuni la ujumla lilitangazwa kwenye tovuti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Julai 2, mwaka 2019 na kurudiwa Desemba 13, na kutangazwa tena katika moja ya magazeti ya serikali.
“Umma uliofahamishwa ni pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, katika mpango wa manunuzi ya jumla ya zabuni 47 zilizoorodheshwa ilijumuishwa ya uchapishaji wa karatasi za kupigia kura. Njia ya kumpata mshindi iliyotangazwa ni ya ushindani wa wazi wa kimataifa,” alifafanua.
Aidha, Dk. Charles alisema ufunguzi wa zabuni ulifanyika Aprili 14, mwaka huu…baada ya uchambuzi, mzabuni Ren-Form CC ilishinda.
Pia alisema kuwa vyama vyote vilishirikishwa katika Kamati ya Kitaifa ya Manunuzi na Lojistiki, na vilishiriki katika hatua zote za manunuzi ya vifaa vya uchaguzi katika dhana ya uwazi na ushirikishwaji.
Alisema vyama vingi ikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) havikuteuwa majina ya wajumbe wa kuandaa kamati ya kitaifa ya manunuzi na lojistiki licha ya kuandikiwa barua Juni 30, mwaka huu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464