Makarani waongozaji wa uchaguzi Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga wakila kiapo leo Oktoba 24, 2020 wilayani kishapu katika kituo cha SHIRECU kwa ajili ya zoezi la uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu. (Picha na Catherine Ngowi).
Na Damian Masyenene, Shinyanga
JUMLA ya makarani waongozaji wa uchaguzi 181 Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga wameapishwa leo Oktoba 24, 2020 katika kituo cha Shirecu wilayani humo na kupewa semina tayari kwa ajili ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 28, mwaka huu.
Makarani hao wameapishwa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kishapu Emmanuel Johnson, ambapo akitoa semina na viapo kwa makarani hao, amewaasa kulinda siri zinazohusu uchaguzi huo, huku akisisitiza kulinda amani ya nchi kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi.
"Hampaswi kutoa matokeo ya uchaguzi kwa mtu yeyote asiyehusika (mtunze siri), kama kuna jambo lolote basi mnapaswa kutoa taarifa kwa tume kupitia utaratibu mlioelekezwa," amesema.
Naye Afisa Msimamizi wa uchaguzi Msaidizi Jimbo la Kishapu, Deus Ngelanizya amewashauri maafisa hao waelekezaji kuwa baada ya kuapishwa ni watumishi wa tume (NEC), hivyo siku ya uchaguzi hawatakiwi kuonyesha misimamo ya vyama vya siasa.
Ngelanizya pia amewataka kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum wakati wa upigaji kura ambao ni wazee, akina mama wajawazito na watu wenye ulemavu kwa kuwaelekeza na kusaidia matumizi ya vifaa mbalimbali vya kupigia kura.