'MCHINA' MBARONI TUHUMA ZA KUMILIKI KIWANDA CHA KUCHENJULIA DHAHABU KAHAMA



Na Salvatory NtanduKahama
Raia wa China, Wang Tao (37) na Yasiri Mussa (26) Mtanzania ambao ni wafanyabiashara wa Madini wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kahama kwa tuhuma ya kumiliki kiwanda cha kuchenjulia dhahabu bila kibali.

Mbele ya Hakimu Makazi wa Mahakama ya Wilaya Davidi Msalilwa,Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi Athumani Kisango amesema kuwa wawili hao wanatuhumiwa kumiliki kiwanda hicho bila kibali kutoka kwa Ofisi ya Madini.

Amesema kuwa Watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Septemba 29, mwaka huu katika eneo la Manzese majira ya usiku ambapo walikamatwa kwa kosa la kumiliki kiwanda hicho kinyume cha sheria ya Madini ya mwaka 2019.

Katika shauri hilo la jinai namba 269 la mwaka huu, Watuhumiwa hao wanadaiwa kukiuka kifungu cha 6 (1) (3)(b)(4) cha sheria ya Madini namba 123 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Watuhumiwa hao wamekana shtaka hilo na shauri hilo limeahirishwa hadi Oktoba 21, mwaka huu litakapotajwa tena mahakamani hapo, hata hivyo wawili hao waliachiliwa huru kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyotolewa na Mahakama hiyo.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464