Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Shinyanga upande wa Uchumi na Uzalishaji, Beda Chamatata (kulia) akimkabidhi hati ya usajili wa Umoja wa vyama vikuu vya ushirika vya Pamba Tanzania (TANCCOPS) jana wakati wa mkutano mkuu wa kwanza wa umoja huo kwenye ukumbi wa SHIRECU mjini Shinyanga
Na Damian Masyenene –Shinyanga
JUMLA ya vyama vikuu vya ushirika vya pamba na vya kati 11 katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Tabora, Katavi na Singida vimeanzisha mradi wa pamoja (Umoja wa vyama vikuu vya ushirika)-TANCCOPS ambao utakuwa chombo cha kukuza uchumi, kupanua ajira na kuunganisha wanachama ambao ni vyama vikuu vya ushirika vya Pamba nchini ili kuwa na nguvu ya uchumi kwa ajili ya kuhudumia wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika vya msingi.
Pia, kuwawezesha kupata pembejeo na zana mbalimbali za kilimo kwa bei nafuu na kwa wakati pia kuongeza thamani na masoko kwa ajili ya mazao yao.
Akiwasilisha taarifa ya uanzishwaji wa TANCCOPS kwenye mkutano mkuu wa kwanza wa umoja huo jana Oktoba 2, 2020 katika ukumbi SHIRECU mjini Shinyanga, Mwenyekiti wa umoja huo, Benjamin Mkomangwa alisema wazo la kuanzisha umoja huo lilibuniwa na wenyeviti na watendaji wa vyama hivyo mwaka jana, ambapo mradi ulianzishwa na kusajiliwa Februari 26, 2020 na kupewa hati yenye namba 5618 kwa mujibu wa sheria ya vyama vya ushirika namba 6 ya mwaka 2013 kifungu cha 33.
Aliwataja wanachama waanzilishi wa umoja huo kuwa ni NCU (Mwanza), SHIRECU (Shinyanga), SIMCU (Simiyu), GCU (Geita), CCU (Chato) Igembe Sabo (Igunga na Nzega), LATCU (Katavi), SIFACU (Singida), M.B.C.U (Bukombe), KACU (Kahama) na CEAMCU (Singida-Manyoni), huku akiiomba serikali kusaidia kuwezesha malipo ya ushuru kwa ushirika (union) na AMCOS na kuharakishwa kwa mchakato wa uagizaji pembejeo ili waweze kukidhi mahitaji halisi ya pembejeo kwa wakulima wao.
“Mradi wetu unatarajia kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kuunda mfuko utaowezesha kuagiza pembejeo za aina mbalimbali za kilimo kwa utaratibu wa manunuzi ya pamoja, uchakataji na utafutaji wa masoko ya amzao, kutoa elimu kwa wakulima na wanachama, kununua na kuchakata zao la pamba na mazao mengine mchanganyiko,” alisema Mkomangwa.
Akieleza mafanikio ya mradi huo hadi sasa, Mkomangwa alisema ni pamoja na uagizaji wa pembejeo uliofanywa na KACU na usambazaji huo kufanywa na vyama vingine vikuu vya ushirika, ununuzi na uchambuaji wa pamba uliofanywa kwa mafanikio na KACU na CCU ulichangia kupanda kwa bei ya Pamba kwa wakulima kutoka bei ya Sh 810 hadi Sh 920 kwa kilo.
“Kuwezekana kwa wakulima kujiunga na huduma ya mfuko wa bima ya afya uliowezeshwa na IgembeSabo na KACU kwa ushirikiano na NHIF na TPB na vyama vikuu vingine vinaendelea na mchakato huu kwa kushirikiana na AMCOS wao. Kuanza kulipwa kwa madai ya wakulima wa pamba msimu wa mwaka 2019 kutokana na malalamiko ya wanachama yaliyopitia umoja huu.
“Tulifanikiwa kupokea viuaduduEkapak2,813,742, Ekapak gawiwa 1,501, 232 na kufanikiwa kubaki na Ekapak 1,312,510, bomba pokelewa ni 19,497, bomba sambazwa 9,397 na bomba zilizobaki kama akiba ni 10,100. Umoja ulisimamia bei ya pamba kutoka Sh 669 iliyopendekezwa na wanunuzi hadi Sh 814 bei elekezi kupitia vikao vya pamoja vya ujengaji wa bei ya pamba,” alisema.
Akizungumza baada ya kukabidhi hati na cheti kwa umoja huo, mgeni rasmi wa kikao hicho, Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Shinyanga- Uchumi na Uzalishaji, Beda Chamatata alisema ili kumaliza changamoto mbalimbali za soko na bei za pamba kwa wakulima na kupata thamani ya mazao, inatakiwa umoja huo upate viwanda vyake vya nyuzi na kuchambua pamba, huku akiahidi kuwa Serikali itawasiliana na bodi ya Pamba kuona namna ya kuharakisha upatikanaji wa mbegu kwa wakulima.
Akiwasilisha taarifa ya ununuzi na uchambuaji wa Pamba, Meneja Uendeshaji wa Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU) ambacho kimekuwa mfano, Amiri Mwinyimkuu alisema walifanikiwa kununua kilo 2,268,670 za Pamba mbegu kutoka wilaya za Kahama, Kishapu na Nyang’wale zenye jumla ya thamani ya Sh 2,044,844,996, ambapo hadi Septemba 30, mwaka huu kiwanda kimeweza kuchambua jumla ya kilo 1,147,600 za pamba mbegu na kuzalisha robota 2,416 zenye wastani wa kilo 181 kwa kila robota na kuzalisha mbegu kiasi cha kilo 667, 936.
“Changamoto ilikuwa kupatikana kwa pamba kidogo kutokana na hali ya hewa baada ya kun yesha mvua kwa muda mrefu hivyo kushindwa kufikia malengo ya ununuzi, kuongezeka gharama za usafirishaji baada ya kulazimika kutafuta pamba nje ya wilaya ya Kahama,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikao hicho, Lenis ambaye pia ni Mwenyekiti wa SHIRECU, aliiomba serikali kuwezesha vyama hivyo viweze kukarabati ginneries kwa sababu kwa sasa kuna uaminifu na vinaweza, hivyo viinuliwe kwani vinabebeka na kwamba mawazo ya ushirika kuna wezi siyo ya kweli, huku akihimiza watendaji wa ushirika kuendelea kuelimisha watumishi wao ngazi zote wadumishe uaminifu ili kukuza ushirika.
Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoa wa Geita, Venance Musiba aliomba vyma hivyo viaminiwe na taasisi za fedha kama ambavyo wanunuzi binafsi wanaaminiwa ili viweze kupata mikopo vinunue pamba nyingi na kufikia malengo, huku Mrajis Msaidizi mkoa wa Geita, Absalom Cheliga akishauri umoja huo kuangalia viwanda vilivyopo na vyenye uwezo na uhitaji wa kufufuliwa ili vitumike kuombea mikopo na kazi zifanyike na mazao ya wakulima yanunuliwe.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Shinyanga upande wa Uchumi na Uzalishaji, Beda Chamatata (kulia) akifungua mkutano mkuu wa kwanza wa TANCCOPS kwenye ukumbi wa SHIRECU mjini Shinyanga, kushoto ni Mwenyekiti wa umoja huo, Benjamin Mkomangwa
Mwenyekiti wa TANCCOPS, Benjamin Mkomangwa (kushoto) akipongezwa na Mwenyekiti wa SHIRECU, Lenis Jishanga baada ya kukabidhiwa hati ya utambulisho wa umoja wa vyama vikuu vya ushirika vya Pamba Tanzania
Mwenyekiti wa TANCCOPS, Benjamin Mkomangwa akionyesha hati na cheti baada ya kukabidhiwa na Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Shinyanga, Beda Chamatata
Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Shinyanga, Beda Chamatata (katikati), Mwenyekiti wa TANCCOPS, Benjamin Mkomangwa (Kushoto) na Mwenyekiti wa mkutano mkuu wa kwanza wa TANCCOPS, Lenis Jishanga (kulia) wakifuatilia hoja mbalimbali za wadau
Mwenyekiti wa TANCCOPS, Benjamin Mkomangwa akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali kwenye mkutano huo
Mwenyekiti wa SHIRECU, Lenis Jishanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa mkutano huo akifafanua jambo
Kaimu Katibu wa SHIRECU, Ramadhan Katto akichangia hoja kwenye mkutano huo
Kikao kikiendelea
Mdau wa TANCCOPS akichangia hoja kwenye mkutano huo
Meneja wa Chama cha Ushirika Chato (CCU), Joseph Masingiri akiwasilisha taarifa ya ununuzi na uchambuaji pamba katika chama chake baada ya kuwa mfano kwenye mradi huo wa pamoja
Chama cha Ushirika Kahama (KACU) ni mfano wa mafanikio ya mradi wa pamoja, ambapo hapa Meneja Uendeshaji wa KACU, Amiri Mwinyimkuu anawasilisha taarifa ya ununuzi na uchambuaji pamba kwa msimu wa mwaka 2019
Meneja wa Chama cha Ushirika mkoa wa Geita (GCU), Venance Musiba akichangia hoja kwenye mkutano huo
Mdau wa zao la Pamba, Joseph Mihangwa akitoa ushauri kwa wanachama wa TANCCOPS
Mrajis Msaidizi M koa wa Singida, Thomas Nyamba akitoa ufafanuzi na ushauri wa mambo mbalimbali kwa vyama vya ushirika
Mrajis Msaidizi mkoa wa Geita, Absalom Cheliga akichangia hoja kwenye mkutano huo
Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wilaya ya Chato (CCU), Deogratias Didi akichangia hoja kwenye mjadala kuhusu kuaminiwa kwa vyama vya ushirika na taasisi za kifedha kwa ajili ya kukopesheka ili kuongeza uwezo wa kununua mazao ya wakulima
Mzee Emmanuel Malunde kutoka chama cha ushirika wilaya za Igunga na Nzega mkoa wa Tabora (IGEMBESABO) akichangia hoja namna ya kufanikisha umoja huo
Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika mkoa wa Mara, Neema Chacha akiwasilisha hoja kwenye mkutano huo
Washiriki wa mkutano huo kutoka mikoa mbalimbali wakifuatilia na kusikiliza mijadala mbalimbali kwenye kikao hicho
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464