MWANAMKE MBARONI KWA KUMKEKETA MJUKUU WA SIKU 9


Detruda Faustine (43), mkazi wa kijiji cha Chibasi Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumkeketa mjukuu wake mwenye umri wa siku tisa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro amewaambia waandishi wa habari leo Alhamisi Oktoba 22, 2020 kuwa mtuhumiwa nadaiwa kutenda kosa hilo Jumanne Oktoba 20, 2020.

“Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote, mara uchunguzi wa awali utakapokamilika, kwa kosa la kumfanyia vitendo vya ukatili mjukuu wake,” amesema Kamanda Muliro

Katika tukio jingine, Kamanda Muliro amesema jeshi hilo linawashikilia viongozi wa watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa tuhuma za kukutwa na kadi 49 za kupigia kura zisizo za kwao kinyume cha kifungu cha 48 (b) cha Sheria ya Uchaguzi sura ya 343 ya 2018.

Amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni Shija Kimwaga, ambaye ni katibu wa Chadema wa kata ya Kabila wilayani Magu, Peter Malemi (mgombea udiwani wa kata hiyo), na Kurwa Patrice.

Wakati huohuo, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa sababu za kifo cha kada wa CCM wa wilaya ya Sengerema, Deogratius Medard kinachohisiwa kusababishwa na chakula kinachodhaniwa kuwa na sumu akiwa katika harakati za kampeni za chama hicho jimbo la Sengerema.

“Kabla ya kufariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitali, Medard anadaiwa kulalamika kuumwa tumbo,” amesema Kamanda Muliro

CHANZO: Mwananchi 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464