Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera amewashauri waangalizi wa ndani wa uchaguzi kuwa na fedha ili wawe na uwezo wa kufanya kazi hiyo badala ya kutegemea wafadhili.
Ametoa kauli hiyo wakati NEC ilipokutana na kufanya mazungumzo na watazamaji wa uchaguzi ndani na nje na kuwaelezea jinsi Tume ilivyojiandaa kwa uchaguzi, wakati wao wakilia na changamoto ya upatikanaji wa fedha.
Akizungumza na wanahabari, Dk Mahera amesema baadhi ya watazamaji wa ndani walisema hawajapata fedha kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya kushiriki uchaguzi.
“Hata sisi wenyewe uchaguzi huu tumetegemea Serikali, hatukuomba fedha nje. Bajeti yetu ilikuwa Sh331 bilioni kwa ajili ya uchaguzi na zote Serikali imetoa na wao sasa hawakupata fedha kutoka kwa wafadhili,” amesema.
“Hivyo watazamaji wa ndani ni vizuri wakati mwingine kujiandaa vizuri kuweza kutafuta fedha kwa ajili ya kutazama na kwa bajeti ambazo ni za kawaida kwa mazingira yetu ya Tanzania ili waweze kutazama uchaguzi na hatimaye kutoa taarifa, kwa hawa watazamaji wa nje wao walikuwa na fedha hawana matatizo yoyote,” amesema Mahera.