Makao Makuu ya Ofisi ya Chadema Kanda ya Serengeti yaliyopo eneo la Majengo Mapya Mjini Shinyanga
Na Shinyanga Press Club Blog
OFISI ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Serengeti inayojumuisha mikoa ya Shinyanga, Mara na Simiyu iliyopo eneo la Ngokolo Manispaa ya Shinyanga, imenusurika kuungua moto baada ya watu wanaodaiwa kuwa na nia ovu kuvamia, kuvunja vioo vya dirisha na kurusha mafuta ya petroli.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Saa 7 usiku wa kuamkia Oktoba 25, mwaka huu, ambapo baada ya waharifu kurusha dumu lenye mafuta ya petroli na kutokomea, moto haukuwaka na ndipo walinzi walipogundua tukio hilo na kutoa taarifa.
Akizungumzia tukio hilo la uvamizi, Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawani alisema walipewa taarifa za tukio hilo na mlinzi na tayari wameripoti shambulio hilo kwa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ambalo limefika eneo la tukio kujionea, huku akieleza kwamba hicho ni kiashiria kibaya kuelekea siku ya uchaguzi.
Mnyawani amedai kuwa tukio hilo ni dalili za hofu ya kushindwa kwa wapinzani wao na kamwe haiwezi kuwasaidia kushinda uchaguzi, bali vyama vinapaswa kunadi sera zao na siyo kufanyiana uhalisi.
"Kuna matukio yanaendelea kutokea tunaona hayana afya kuelekea siku ya kupiga kura.....Ofisi yetu imenusurika na shambulio la kuchomwa moto baada ya mharifu kuvunja kioo cha dirisha la Ofisi ya katibu na kurusha ndani kidumu cha lita 1.5 ya mafuta ya petroli lakini bahati nzuri moto haukuwaka kwa sababu kilikuwa kimefungwa.
"Tumetoa taarifa Polisi na tunashukuru uongozi wa jeshi hilo ngazi ya wilaya na mkoa kwa ushirikiano waliouonyesha hadi sasa, kwa sababu baada ya kupata taarifa OCD (mkuu wa polisi wilaya) na RCO (Mkuu wa upelelezi mkoa) walifika kujionea hali halisi na tunawapongeza kwa hatua walizochukua hadi sasa," amesema.
Mwandishi wetu ameshuhudia Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Shinyanga, Davis Msangi akiwa eneo la tukio kwa ukaguzi na kushuhudia kilichotokea katika ofisi hiyo.
RPC AELEZA
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba amesema jeshi lake linaendelea na uchunguzi wa tukio la kuvunja ofisi ya Chadema Kanda ya Serengeti iliyopo Majengo Mapya mjini Shinyanga.
Kamanda Magiligimba ameeleza kuwa mnamo Oktoba 25, mwaka huu majira ya saa 10 alfajiri katika ofisi za Chadema Kanda ya Serengeti zilizopo Majengo Mapya, Kata ya Ngokolo, Joseph Ndatala, (43) ambaye ni Afisa uendeshaji, mipango na uchaguzi Chadema mkazi wa Ndala aligundua kioo cha dirisha la ofisi ya ofisa wa ‘organization’ na uchaguzi kuvunjwa na mtu/watu ambao bado hawajafahamika.
“Katika eneo la tukio kumekutwa chupa moja yenye ujazo wa lita 1.5 yenye kimiminika kidhaniwacho ni mafuta ya petrol ndani yake ikiwa na utambi.
mtuhumiwa mmoja anashikiliwa kwa mahojiano zaidi ambae ni Edward Andrea (46) ambaye ni mlinzi wa Shiroh Security Ltd,” amesema.
Kamanda huyo ametoa natoa wito kwa wanasiasa pamoja na wafuasi wao kuacha kufanya siasa za vurugu hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi na wafanye kampeni zao kwa amani na utulivu na mara baada ya mikutano kumalizika wananchi wanatakiwa kutawanyika na si kufanya maandamano kuelekea kokote kule.
WAMUOMBA IGP SIRRO
Katika hatua nyingine, Katibu huyo wa Chadema, Mnyawani amemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro kuingilia kati na kuwawajibisha baadhi ya wakuu wa polisi katika vituo mbalimbali kwenye mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu anaodai wanawakamata mawakala na viongozi wa chama hicho ili kuvuruga uchaguzi mkuu.
Mnyawani amedai kuwa kumekuwa na operesheni kabambe ya kuwakamata mawakala wao, ambao ametoa wito mawakala hao waachiwe ama kama wana kesi basi wafikishwe mahakamani ili wapate dhamana.
"Tunatoa wito mawakala wetu waachiwe kabla ya siku ya uchaguzi, vinginevyo vituo hivyo havitafanya uchaguzi, mpaka sasa Bariadi wamekamatwa wanne, Serengeti watatu na Rorya pia, hakuna kituo kitaendelea na uchaguzi kama mawakala wetu hawataachiwa....tunaomba IGP aingilie kati azuie matukio haya ya ukamataji.
"Lakini pia kuna wasimamizi wa uchaguzi wamekataa kuwaapisha mawakala wetu hata baada ya Tume kuongeza muda, tunaomba sana waapishwe," amesema.
CHADEMA YASISITIZA KULINDA KURA
Akizungumzia kuhusu kulinda kura, Mnyawani alisema kuwa msimamo wa chama chao uko pale pale, ambapo baada ya kupiga kura lazima wazilinde na kuwalinda mawakala wao ili wasidhurike.
"Msimamo wetu upo pale pale, piga kura linda kura na mlinde wakala,...wanaotaka tusilinde kura ndiyo hao wamejiandaa kuiba kura, tunafanya hivyo kulinda mawakala wasidhurike kwahiyo tutawalinda mawakala wetu kwa nguvu na gharama yoyote ili wasitolewe vituoni kwa hujuma," amesistiza.
Mabaki ya vioo vilivyovunjwa wakati wa uvamizi huo
Sehemu ya dirisha lililovunjwa wakati wa uvamizi huo
Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawani akizungumza na waandishi wa habari mapema leo juu ya tukio la shambulio la kutaka kuchoma ofisi za chama hicho.
Picha na Marco Maduhu