Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga (hawapo pichani) leo Oktoba 24, 2020 juu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, 2020 Jumatano ya wiki ijayo.
Na Damian Masyenene, Shinyanga
ZIKIWA zimebaki siku nne ili Watanzania wafanye maamuzi ya kuwachagua viongozi wawatakao siku ya Jumatano ya Oktoba 28, mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack amewahikikishia usalama wakazi wa mkoa huo kwa kuwaeleza kwamba ulinzi umeimarishwa na hakuna mwananchi hata mmoja atakayejeruhiwa ama kudhurika kutokana na zoezi hilo la upigaji kura.
RC Telack amesisitiza kwa kusema kuwa mkoa wake unatarajia kuwa na uchaguzi ambao hautaacha jeraha kwa mtu yeyote, ambapo wamehakikisha kunakuwa na mazingira bora ya kufanya wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida baada ya zoezi la upigaji kura.
Mkuu huyo wa mkoa ameyasema hayo leo Oktoba 24, 2020 ofisini kwake katika mkutano na waandishi wa habari mjini Shinyanga, huku akiwasihi wanahabari kutoingilia majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kutangaza matokeo kwa mihemko na kuleta sintofahamu kwa jamii.
“Mkoa tumejipanga kuhakikisha kwamba hajeruhiwi mtu yeyote na hakuna atakayedhurika kwa namna yoyote kwa sababu ya uchaguzi, niwahakikishie kwamba usalama utakuwepo wa kutosha na tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba watu wote wanaotakiwa kupiga kura watatimiza haki yao na shughuli zingine zitaendelea,” amesema.
Katika hatua nyingine, RC Telack amewaonya wote wenye nia ovu ya kuleta vurugu kwa madai ya kulinda kura, huku akiwahakikishia wananchi kwamba hakutakuwa na kura yoyote itakayoibwa, na wenye jukumu la kulinda kura ni mawakala na siyo wapiga kura ama wananchi.
“Baada ya kupiga kura wananchi wote warudi nyumbani wakaendelee na shughuli nyingine, wanaojiandaa kuvuruga zoezi hili waache mara moja, matokeo yatatangazwa kwa mujibu wa sheria……wanaosema watalinda kura naomba wasilinde kwa sababu hakuna ambaye ataiba kura na wala wasiwe na wasiwasi, tayari kuna mawakala watafanya shughuli hiyo,” amesisitiza RC Telack.
Ameongeza kwa kueleza kuwa vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1 asubuhi hadi saa 10 jioni, hivyo wapiga kura wawahi kwenye vituo kuepusha msongamano, huku pia akiwaomba wananchi wa mkoa wa Shinyanga wenye sifa za kupiga kura wajitokeze kuchagua viongozi wanaowataka.
Kwa upande wake, Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Shinyanga, Fabian Kamoga ameeleza kuwa tayari vifaa vya kupigia kura vimekwishapokelewa na wanasubiri kuanza kuvisambaza kwenye maeneo husika, ambapo mkoa huo unavyo vituo 2,700 vya kupigia kura, ambapo kila kituo kitakuwa na watendaji wane na mlinzi mmoja.
Pia amesisitiza kwa kuwataka wananchi kujiepusha na mavazi yanayoashiria itikadi ya vyama vya siasa siku ya upigaji kura.
RC Telack akisisitiza jambo kwenye kikao chake na waandishi wa habari, leo.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo
Kikao kikiendelea
Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Shinyanga, Fabian Kamoga akifafanua mambo mbalimbali mbele ya waandishi wa habari
waandishi wa habari wakifuatilia kikao chao na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
Waandishi wa habari wakimsikiliza RC Telack
Kikao kikiendelea
Jengo la ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464