Sangara
KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dk Rashid Tamatamah amewataka wafugaji na wavuvi watumie teknolojia zilizopo kuzalishaji kwenye mifugo, uvuvi na ukuzaji viumbe maji ili wapate faida.
Amebainisha kuwa sekta za uvuvi na mifugo zimekua katika mwaka wa fedha 2019/20 na kuchangia zaidi kwenye pato la taifa.
Dk Tamatamah aliyasema hayo kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kitaifa mkoani Njombe. Kilele cha maadhimisho hayo ni Oktoba 16 mwaka huu.
Alisema katika mwaka 2019/20, sekta ya uvuvi ilikua kwa kiwango cha asilimia 1.5 na kuchangia Pato la Taifa (GDP) kwa asilimia 1.71.
“Vile vile, kumekuwepo na ongezeko la uwingi wa samaki katika maji yetu hususani katika Ziwa Victoria ambapo samaki aina ya sangara wameongezeka kutoka tani 417,936 mwaka 2016 hadi tani 816,964 mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 95.5,” alisema Dk Tamatamah.
Alisema, uzalishaji na uvunaji wa samaki katika maji ya asili umeongezeka kutoka tani 362,645 mwaka 2015/2016 hadi tani 497,567 mwaka 2019/2020 na pia uzalishaji wa mazao ya viumbe maji kufikia tani 18,716.56.
Dk Tamatamah alisema kwa kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi mwaka 2019/2020, tasnia ya ukuzaji viumbe maji imekua na kwamba, idadi ya mabwawa ya samaki imeongezeka kutoka 22,545 hadi 26,445, vizimba kutoka 109 hadi 431.
Alisema wastani wa ulaji wa samaki kwa mtu kwa mwaka nchini umeongezeka kutoka kilo 8.2 mwaka 2018/2019 hadi kufikia kilo 8.5 mwaka 2019/2020.
Aidha, kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa ulaji samaki duniani ni kilo 20.3 kwa mtu kwa mwaka.
Kuhusu mifugo, Dk Tamatamah alisema sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kuwapatia wananchi ajira, chakula, lishe, kipato na fedha za kigeni.
Alisema katika mwaka 2019/2020, sekta hiyo ilichangia asilimia 7.4 katika Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 7.2 mwaka 2018/2019. Pia, imekua kwa asilimia tano kwa mwaka 2019/2020 ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka 2018/2019.
Dk Tamatamah alieleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2019/2020 uzalishaji wa maziwa ulifikia lita bilioni 3.0 ukilinganisha na lita bilioni 2.7 zilizozalishwa katika kipindi cha mwaka 2018/2019.
“Ongezeko la uzalishaji limetokana na ongezeko la ng’ombe na kuboreshwa kwa mazingira ya uwekezaji katika tasnia ya maziwa nchini. Pia uzalishaji wa zao la nyama umeongezeka kufikia tani 701, 679.1 katika kipindi cha mwaka 2019/2020 tofauti na tani 690,629 zilizozalishwa mwaka 2018/201,” alisema Dk Tamatamah.
Alisema pamoja na ongezeko hilo, bado ulaji wa nyama na maziwa nchini si wa kuridhisha.“Niendelee kutoa rai kwa wananchi kuongeza ulaji wa nyama ili tuweze kufikia kiwango kilichosimikwa na Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO) cha kilo 50 kwa mwaka kwa mtu mmoja na unywaji wa maziwa kufikia lita 200 kwa mtu kwa mwaka,” alisema.
Alisema pia uzalishaji wa mayai uliongezeka nchini kutoka mayai bilioni 3.58 mwaka 2018/2019 hadi bilioni 4.05 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 13.3.
“Ongezeko hili la mazao ya mifugo na uvuvi limetokana na dhamira ya serikali katika kuhakikisha kuwa wananchi wake wanaondokana na tatizo la uhaba wa chakula nchini hususan katika suala la upatikanaji wa protini ya samaki na nyama,” alisema Dk Tamatamah.