TAHADHARI DHIDI YA CORONA YATAKIWA KUCHUKULIWA MIKUTANO YA KAMPENI


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kahama, Thomas Myonga akizungumza na wananchi wa kata ya Sabasabini

Na Salvatory Ntandu-Kahama
Katika jitihada za kupambana na ugonjwa wa homa kali ya Mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona,Wananchi wanaoshiriki katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu, wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga ugonjwa huo ni pamoja na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Kahama, Thomas Myonga katika mkutano wa kampeni za kumnadi mgombea Udiwani wa Kata ya Sabasabini, Emmanuel Makashi uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Sabasabini, ambapo alisema kuwa virusi vya Corona bado vipo hivyo ni vyema kila mwananchi achukue tahadhari.

Alisema kuwa katika mikutano ya kamapeni za vyama vya siasa mbalimbali kuna mikusanyiko mikubwa ya watu, hivyo ni vyema wakachukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji safi na sabuni ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa COVID 19.

“Tumefanya Maombi ya Kitaifa ya siku tatu na Ugonjwa Corona umeisha hapa nchini tukiongozwa na Rais wetu Dk John Pombe Magufuli Mwenyekiti wetu wa (CCM) Taifa, hivyo ni bora tukaendelea kuchukua tadhari dhidi ya janga hili ambalo limeutikisa ulimwengu,”alisema Myonga.

Maduka Nyanda ni Mfanyabiashara katika kata ya sababini alisema kuwa kuwa bado wanaendelea kuzingatia maelekezo ya serikali ikiwa ni pamoja na kuweka ndoo za kunawia mikono katika maduka yao ili wateja waweze kunawa kabla ya kupatiwa huduma ili kujikinga na mambukizi ya Covid 19.

“Japo kuna wengine hawapendi kunawa mikono nje ya Maduka yetu kwa dhana potofu ya kuwa Corona imekwisha isha jambo ambalo linapaswa kukemewa mara moja kwani Ugonjwa huu ukichukua tadhari hauwezi kuleta Madhara kwa wananchi,”alisema Nyanda.

Victorina Elias Mtaalamu wa afya ambaye ni Muuzaji wa Duka la Dawa Muhimu katika kata ya Sababini alisema kuwa jamii bado inahitaji elimu zaidi ili kujikinga na Corona kutokana na baadhi ya wananchi kuendelea kupuuza maelekezo ya serikali dhidi ya Janga hili ambalo linaendelea kuleta madhara kwa watu wasiozingatia maelekezo ya Serikali.

“Serikali inapaswa kuendelea kutoa elimu kwa njia shirikishi kwa wananchi kwa kutumia vyombo vya habari ili waposhiriki mikutano ya kampeni wasikae kwa kubanana ili kuzuia kusambaa kwa maambukizi endapo miongoni mwa watu wanaoshiriki katika kampeni hizo ni mgonjwa,”alisema Elias.

Mahembe Malanduja ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Sabasabini alisema kuwa bado wanaendelea kutoa elimu kwenye jamii kwa kushirikiana na wataalamu wa afya waliopo katika ngazi ya kata kupitia mikutano ya hadhara ili kujikinga na ugonjwa huo hatari ambao atahari zake ni kubwa pindi mwananchi anapougua.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464