VIJANA WAWILI WADAKWA KWA KUMBAKA MTOTO WA MIAKA 6 WAKIMRUBUNI KWA PIPI


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Debora Magiligimba

Na Damian Masyenene –Shinyanga
WAKATI Mkoa wa Shinyanga ukizindua mpango mkakati wa kipekee wa miaka mitano (2020-2025) wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, ukiwa ni mkoa wa kwanza nchini kuja na mpango huo, vitendo hivyo vimeendelea kuripotiwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Ambapo Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linawashikilia vijana wawili wenye miaka 14 kila mmoja kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka sita kwa tamaa za kingono.

Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la polisi ambayo imetolewa leo Oktoba 15, 2020 kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba, imewataja watuhumiwa hao kuwa ni Jakaya john (14) na Boaz Shija (14) wote wakazi wa mtaa wa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 6.

Akielezea tukio hilo, Kamanda Magiligimba ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 12, mwaka huu saa 2:45 usiku katika Mtaa na Kata ya Ndembezi, Manispaa na Mkoa wa Shinyanga, ambapo mama wa mtoto huyo (Jina linahifadhiwa) aligundua kubakwa kwa mtoto wake na watuhumiwa hao wawili baada ya kumlaghai mtoto huyo kwa kumnunulia pipi na kumpa hela kisha kumpeleka eneo la vichaka lililopo karibu na nyumbani kwa mtoto huyo.

Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Natoa wito kwa wazazi/walezi kwa pamoja kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la p
olisi ili vitendo hivi vya ukatili dhidi ya watoto vikomeshwe,” amesema ACP Magiligimba. 

Kuzinduliwa kwa mpango mkakati huo huenda ikawa suluhisho la vitendo hivi vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, endapo kila mdau atatimiza wajibu wake na kuhakikisha watuhumiwa wanafikishwa kwenye mikono ya sheria na kutoa funzo kwa wengine wenye nia ovu ya kutekeleza vitendo hivyo.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464