Baadhi ya wakazi wa mji mdogo wa Isaka wilayani Kahama wakichota maji katika Kioski kilichojengwa kuhudumia wananchi kwenye mradi mkubwa wa maji safi na salama kutoka Ziwa Viktoria wa Isaka–Kagongwa uliogharimu Sh Bilioni 24.7
Na Damian Masyenene –Shinyanga
JUMLA ya wakazi 95,000 wanaoishi kwenye miji midogo ya Isaka na Kagongwa pamoja na vijiji vya Kitwana na Ngogwa wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga wanatarajiwa kupata huduma ya maji safi na salama kutoka Ziwa Viktoria baada ya kukamilika kwa miradi ya maji iliyogharimu Sh Bilioni 27.1.
Miradi hiyo ni ule wa Isaka–Kagongwa uliogharimu Sh Bilioni 24.7 ambayo tayari umekamilika tangu Septemba, 2019 na umeanza kutoa huduma kwa wananchi, ambapo jumla ya wakazi 817 wa miji hiyo midogo wameunganishwa na huduma ya maji safi na salama kutoka Ziwa Viktoria tangu ulipoanza kazi Septemba mwaka jana, ambapo Isaka inao wakazi 16,000 na Kagongwa 35,000.
Katika mradi wa Kitwana–Ngogwa ambao umegharimu Sh Bilioni 2.4 ukiwa na matanki mawili yenye ujazo wa lita 135,000 (Kitwana) na 680,000 (Ngongwa) yakiwa yamejengwa kwa Sh Milioni 350 kila moja, ulianza kujengwa Juni mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Novemba, mwaka huu ukikusudiwa kuwahudumia wananchi 44,000 katika vijiji hivyo kwa kuunganishiwa huduma majumbani na kwenye Vioski pamoja na kujengewa maeneo ya kunyweshea mifugo ili kuepuka uharibifu wa miundombinu.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 6, 2020 katika ziara ya wataalam kutoka Wizara ya Maji wakiongozwa na Mhasibu Mkuu wa wizara hiyo, Ahadi Msangi walipotembelea miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa na Serikali mkoani Shinyanga kupitia mamlaka za maji za Kahama na Shinyanga (KASHUWASA), Mjini Shinyanga (SHUWASA) na mjini Kahama (KUWASA).
Mkuu wa msafara wa wataalam kutoka wizara ya maji, Mhasibu Mkuu wa wizara hiyo, Ahadi Msangi ameahidi kushughulikia changamoto zilizobainishwa ikiwemo gharama zilizoongezeka za kuunganisha wateja, huku akisisitiza wananchi kuelimishwa ili waunganishwe kwenye mtandao wa maji safi na salama ambayo yameletwa kwa ajili yao.
“Mradi huu lengo ni kuwahudumia wananchi kwa maji safi kutoka Ziwa Viktoria na kiasi kikubwa cha fedha kimetumika kuukamilisha, kwahiyo bado kuna nafasi kubwa ya watu kuingia kwenye mtandao huu wa maji na waendelee kuhamasishwa…..miji hii (Kagongwa na Isaka) ina takribani watu 50,000 na kabla ya mradi huu ni kama asilimia tisa ya watu waliokuwa wanapata maji safi lakini sasa tunaona wananchi wengi watanufaika,” alisema.
Meneja wa Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Julieth Payovela akitoa taarifa ya upatikanaji maji katika mkoa huo wenye wakazi zaidi ya Milioni 1 huku asilimia 79.5 ya wakazi wake wakiwa vijijini na 20.5 mjini, alisema kuwa hadi Septemba, mwaka huu upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini ni asilimia 60.03 na mijini asilimia 70, na upatikanaji wa jumla wa maji safi na salama mkoani hapa ni asilimia 66.1 kupitia mamlaka tatu za KASHUWASA, SHUWASA na KUWASA.
“Baadhi ya changamoto zinazotukabili katika kutoa huduma mkoani kwetu ni pamoja na kutopatikana kwa vyanzo vya uhakika vya maji kwenye maeneo, upungufu wa watumishi kwenye mamlaka zetu, ucheleweshaji malipo ya wakandarasi, na kukosekana kwa mfumo wa majitaka katika manispaa ya Shinyanga na Mji wa Kahama, hivyo tunaiomba Serikali kutoa fedha kwa wakati ili miradi husika iweze kukamilika kwa wakati,” alisema.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa Isaka–Kagongwa wilayani Kahama ulioanza kujengwa Julai, 2017 na kumalizika Septemba, 2019, Meneja Ufundi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Kahama (KUWASA), Mhandisi Paul Luchanganya amesema baada ya kukamilika mradi huo walikabidhiwa na KASHUWASA kwa ajili ya kuuendesha na lengo lilikuwa kuunganisha wateja 2,000 katika miji ya Isaka na Kagongwa.
Mhandisi Luchanganya ameeleza kuwa kila mji ulikuwa na lengo la kuunganishiwa wateja 1,000 , ambapo jumla ya wateja 446 wameunganishwa na huduma ya maji safi katika mji mdogo wa Isaka, huku 371 wakiunganishwa Kagongwa.
“Kuna changamoto kadhaa ambapo tunalazimika kuongeza huduma kwa wateja ambao sasa wamekuwa mbali tofauti na matarajio yetu kwa hiyo bajeti inatubana na gharama zimeongezeka, mfano hapa Isaka zinahitajika mabomba madogo ya inchi mbili yenye urefu wa Km 17 na Kagongwa Km 8 kuwafikia wananchi.
“Tatizo lingine linalofanya tusifikie lengo ni wananchi wengi wana vyanzo vyao vya maji kama vile visima kwahiyo hawaoni umuhimu wa kujiunga na huduma hii, kwahiyo tunaendelea kutoa elimu na kuhamasisha kwa sababu serikali imewasogezea huduma karibu na maji ni safi na salama,” alisema.
Akielezea utekelezaji wa mradi mwingine wa maji wa Kitwana –Ngogwa wilayani Kahama uliotembelewa na wataalam hao, Mhandisi wa Mipango na Ujenzi Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Kahama (KUWASA), Magige Marwa alisema mradi huo umegharimu Sh Bilioni 2.4 ukiwa na matanki mawili yenye ujazo wa lita 135,000 (Kitwana) na 680,000 (Ngongwa) yakiwa yamejengwa kwa Sh Milioni 350 kila moja.
Mradi huo ulianza kujengwa Juni mwaka huu na unatarajiwa kukamilika Novemba, mwaka huu ukikusudiwa kuwahudumia wananchi 44,000 katika vijiji hivyo kwa kuunganishiwa huduma majumbani na kwenye Vioski pamoja na kujengewa maeneo ya kunyweshea mifugo ili kuepuka uharibifu wa miundombinu.
Timu hiyo ya wataalam ilitembelea pia mradi wa maji Mwanva–Mbulu mjini Kahama ambao una mtandao wa Km 15.7 za mabomba uliogharimu Sh Milioni 686 ukilenga kunufaisha wananchi 10,000 katika vijiji hivyo pale utakapokamilika.
Baadhi ya wakazi wa maeneo ya Isaka na Kitwana, akiwemo
Sadick Juma na Catherine Sylivester wamesema kuwa ujio wa miradi hiyo ni
mkombozi kwani walikuwa wanahangaika kupata maji safi, huku wakiuziwa maji kwa
gharama kubwa ya Sh 500 ndoo na Sh 3,000 pipa moja ambayo ni maji ya visimani.
“Hapa kitongoji cha Sofi kata Mongolo Kahama tuna furaha
maji sasa tunayapata nyumbani, lakini zamani tulikuwa tunapata tabu sana
tunanunua maji ya visima tena kijiji jirani kwa kuuziwa pipa moja Sh 3,000 na
ulikuwa unaondoka asubuhi saa mbili unarudi mchana saa 8, baada ya hili naomba
sasa tusogezewe na huduma ya umeme,” amesema.
Mhasibu Mkuu Wizara ya Maji, Ahadi Msangi (kulia) akizungumza na baadhi ya wananchi katika mji mdogo wa Isaka wilayani Kahama waliokuwa wanachota maji safi na salama katika kioski kilichojengwa na mradi wa Isaka –Kagongwa
Meneja wa Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (RUWASA) mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Julieth Payovela (kushoto) akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama mkoa wa Shinyanga mbele ya jopo la wataalam kutoka wizara ya maji waliotembelea kukagua miradi mbalimbali
Meneja Ufundi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Kahama (KUWASA), Mhandisi Paul Luchanganya akitoa maelezo mbele ya wataalam wa wizara ya maji na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa mradi wa Isaka–Kagongwa
Wataalam kutoka Wizara ya Maji wakiongozwa na Mhasibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ahadi Msangi (katikati aliyevaa miwani) wakipata maelezo kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali wilayani Kahama
Meneja Mipango na Ujenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Kahama (KUWASA), Mhandisi Magige Marwa akiulezea mradi wa Kitwana–Ngogwa utakaohudumia wananchi 44,000 utakapokamilika mwezi Novemba, mwaka huu
Ukaguzi wa maeneo na miundombinu ya mradi wa Kitwana–Ngogwa ukiendelea
Sehemu ya mabomba yatakayotumika kusafirisha maji kwenda kwa wananchi wa vijiji vya Kitwana na Ngogwa wilayani Kahama
Matanki mawili yenye mita za ujazo 800 kila moja yaliyojengwa katika mji wa Kagongwa ambayo yanatumika kusambaza maji kwa wananchi katika miji midogo ya Kagongwa na Isaka wilayani Kahama
Tanki la maji lenye ujazo wa lita 135,000 linalojengwa katika kijiji cha Kitwana wilayani Kahama ambalo ni sehemu ya mradi wa maji Kitwana–Ngogwa utakaohudumia wananchi 44,000 utakapokamilika mwezi Novemba mwaka huu
Mabomba yanayotumika kuwaunganishia wananchi na huduma ya maji katika miji midogo ya Isaka na Kagongwa
Mkazi wa kitongoji cha Sofi kata ya Mongolo mjini Kahama, Catherine Sylivester ambaye tayari ameunganishwa na huduma ya maji kwenye mradi wa Kitwana –Ngogwa akielezea hali ilivyokuwa awali kabla ya kusogezewa huduma hiyo
Picha ya pamoja ya wataalam kutoka wizara ya maji na mamlaka za Maji za SHUWASA na KUWASA katika eneo yalipojengwa matanki mawili ya maji katika mji mdogo wa Kagongwa wilayani Kahama
Picha na Marco Maduhu