Mtaalam wa Usalama na Afya ya Kimataifa, Dk. Onesmo Mwegoha ambaye pia ni Daktari wa binadamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga katika moja ya majukumu yake akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari wa mkoa huo juu ya magonjwa ya mlipuko
Na Chibura Makorongo, Shinyanga
LICHA ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Septemba 23, mwaka huu kueleza kupungua kwa kasi ya magonjwa ya mlipuko hususani
kipindupindu hapa nchini, wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wametakiwa kuhakikisha wanazingatia elimu na tahadhari zinazotolewa na wataalamu wa afya kitengo cha elimu kwa umma kuhusu magonjwa ya mlipuko na mengine ili kuepusha madhara mbalimbali yanayoweza kujitokeza.
Wito huo umetolewa na Afisa Afya Manispaa ya Shinyanga, Sanya Mwara wakati akizungumza na Shinyanga Press Club Blog ofisini kwake juu ya namna idara yake inavyotoa elimu kwa wananchi wa manispaa hiyo kuhusu ya magonjwa ya mlipuko na mengineyo.
Sanya ameeleza kuwa vituo vya afya na zahanati vilivyoko ndani ya manispaa huwa na utaratibu wa kutoa ripoti kila wiki ya wagonjwa wanaoripoti na aina ya magonjwa yanayowakabili, na kunapo tokea kukaonekana ugonjwa umevuka kiwango cha kitaalam ndipo idara hiyo kupitia kitengo cha elimu ya umma hufuatilia kwa ajili ya kutoa elimu ya kujikinga na madhara yake.
"Kitengo hiki kiko kwa mujibu wa sheria za afya na kina fanya kazi kila wakati isipo kuwa watu wetu wanapo alikwa na viongozi wa mitaa muitikio unakuwa mdogo, linapotokea athari tuna nyooshewa vidole haswa kwa wanoishi mijini ambao hujali shughuli zao sana,
"Ufike wakati Watanzania waumizwe na kodi zao kwa kujua serikali inatumia pesa nyingi kutibu binadamu haswa kwa magonjwa haya yasiyo ambukiza, kujikinga ni bora waache kupuuzia wanapoitwa waje kusikiliza kwa manufaa yao" amesema Sanya.
Kwa upande wake, Mtaalam wa Usalama na Afya ya Kimataifa, Dk. Onesmo Mwegoha ambaye pia ni Daktari wa binadamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, amesema magonjwa ya mlipuko ni hatari zaidi, kutokana na ufugaji wanyamapori usiozingatia utaalam ambapo binadamu hulazimika kuchangamana na wanyama kwa kiasi kikubwa.
Amesema kuwa kitendo cha binadamu kuamua kuwazoea na kuanza kuwafuga na kuchangamana na wanyamapori ni moja ya sababu inayofanya binadamu waambukizwe magonjwa ya mlipuko kwa urahisi.
"Lakini pia mazoea ya baadhi ya watu kutonawa mikono kwa sabuni baada ya kugusana na wanyama au wanapowahudumia kwa kuwapatia chakula wanyama, hupelekea kuambukizwa magonjwa na kuyasambaza kwa watu wengine," amebainisha.
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga akiwemo Juma Athumani na Mary Mhoja, wakizungumzia namna wanavyozingatia elimu inayotolewa na wataalam wa afya, wameeleza kuwa changamoto za kazi na utafutaji wa riziki umewafanya watu wengi kutofuatilia elimu inayotolewa kwa umma.
"Mfano kama sisi mama lishe muda wote tunakuwa kwenye shughuli tunaondoka alfajiri nyumbani na kurudi usiku, kwahiyo hata kama kuna watu wanakuja kutoa semina tunapitwa kwa kukosa taarifa," amesema Mary.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464