WATUMISHI TUME YA MADINI WATAKIWA KUWA NA UADILIFU KAZINI KUVUTIA UWEKEZAJI



Na Greyson Mwase
Watumishi wa Tume ya Madini nchini wametakiwa kuwa waadilifu kwenye utendaji wa shughuli zao za kila siku hivyo kuendelea kujenga taswira chanya kwenye Sekta ya Madini.

Wito huo umetolewa leo tarehe 22 Oktoba, 2020 na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya kwenye ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua shughuli za Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mbeya pamoja na kutatua changamoto mbalimbali.

Katika ziara yake Profesa Manya ameambatana na Meneja Utawala na Rasilimaliwatu, Gift Kilimwomeshi na kupokelewa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mbeya, Godson Kamihanda.

Akizungumza na watumishi hao, Profesa Manya amesema kuwa, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imejipanga katika kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye Sekta ya Madini, na kusisitiza kuwa uadilifu kwenye utendaji kazi unahitajika ili kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye Sekta ya Madini.

Katika hatua nyingine, Profesa Manya amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa weledi ili kujenga jina zuri la Tume ya Madini.

Ziara hii ni sehemu ya ziara ya Profesa Manya katika Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa Nchini yenye lengo la kukagua utendaji wa Ofisi za Madini, kusikiliza changamoto za watumishi na kuzitatua huku elimu kuhusu utumishi wa umma na maelekezo mbalimbali yakitolewa.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa ofisi hiyo katika mahojiano maalum, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mbeya, Godson Kamihanda amesema kuwa wamefarijika na ujio wa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kwenye ofisi hiyo na kuahidi kufanyia kazi maelekezo yaliyotolewa.

"Tunashukuru na kumpongeza sana Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya na Meneja Utawala na Rasilimaliwatu, Gift Kilimwomeshi kwa kututembelea na kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinatukabili pamoja na kutupa ufafanuzi wa miongozo mbalimbali kwenye utendaji wa shughuli za Serikali, ninaamini elimu kubwa waliyotupa itatusaidia kutatua changamoto ndogo zilizokuwa zinatukabili," amesisitiza Kamihanda. 



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464