WAZAZI MSALALA WAONYWA KUWAOGESHA WATOTO WA KIKE DAWA ZA MVUTO WA MAPENZI


Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Ntanwa Kilagwile (aliyesimama) akizungumza jana katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike Duniani yaliyofanyika kiwilaya yviwanja vya Shule ya Msingi Segese

Na Salvatory Ntandu -Kahama
Katika Jitihada za kukabiliana na Mila na tamaduni potofu zilizopitwa na wakati katika halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga, jamii za wafugaji zimetakiwa kuacha tabia za kuwaogesha dawa za mvuto watoto wake.

Hayo yalibainishwa jana Oktoba 11, 2020 na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Ntanwa Kilagwile katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike Duniani ambapo kiwilaya yalifanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Segese.

Alisema kuwa jamii za wafugaji katika maeneo ya vijijini bado zinaendekeza mila hizo potofu ambapo watoto wakike hususani wanafunzi wenye umri wa chini ya miaka18 huogeshwa dawa za kuongeza mvuto wa mapenzi hali ambayo imetajwa kuchochea kujihusisha na mapenzi.

Alifafanua kuwa, wanafunzi wengi wamekuwa wakiogeshwa na kuchanjwa dawa za mvuto wa mapenzi ni wale wenye umri kati ya miaka 16 hadi 18 na hiyo imekuwa kisababishia kushindwa kufanya vema kwenye mitihani yao ya mwisho kutokana na kuwaza kuolewa baada ya kuoga dawa hizo.

“Sisi kama Halmashauri tunalikemea sana jambo hili na ndio maana tunajenga mabweni ya watoto wa kike na mabweni manne kati ya sita tuliojenga yanatumia….hivi sasa tunatarajia kujenga shule ya sekondari kwa ajilii ya wanafunzi wa kike kama moja ya kupamba na hili,” amesema Kilagwile.

Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo, Neema Katengesya, alisema kuwa hakuna dawa ya kuondoa mikosa ya mapenzi,mikosi mingine inajitokeza pale mwanamke au binti anapokuwa anajipitsha kwa wanaume ili aitwe na kutongozwa.

Aidha aliongeza kwa kueleza kuwa wameanza kutunga sheria ndogo za Halmashauri itakayomtaka mtoto wa kike hasa mwanafunzi kutotembea kwenye mikusanyiko ya watu ikiwemo kwenye magulio na minada ili kumepusha na vishawishi ambavyo vinaweza kusababisha akapata mimba akiwa shuleni.

Kwa upande wake Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Nancy Sumari ambae alikuwa Miss Tanzania Mwaka 2005, alisema kuwa kila mzazi anatakiwa kujenga desturi ya kuzungumza na mtoto wake wa kike kirafiki na kutatua changamoto alizonazo ambazo zitamuepusha kuingia kwenye vishawishi.

Nancy alisema kuwa mtoto wa kike anamahitaji mengi ukilinganisha na mtoto wa kiume, asilimia kubwa wengi wao wanaingia kwenye vishawishi vinavyosababisha kukatisha ndoto zao baada ya mzazi kutoshiriki kikamilifu katika kutatua changamoto alizonazo binti yake.

Mmoja wa wanafunzi ambae hakutaka jina lake kutajwa, alidai kuwa wazazi wamekuwa wakiwalazimisha kuwapeleka kwa waganga wa jadi kuwaogesha dawa za mvuto wa mapenzi na kuomba elimu iendelee kutolewa kwa wazazi ili kuwaondolea dhana hiyo vichwani mwao. 

 Baadhi ya wanafunzi wa kike waliohudhuria maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani, ambayo kwa wilaya ya Kahama yalifanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Segese halmashauri ya Msalala.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464