WAZEE 13,427 WILAYA YA SHINYANGA KUPATA AHUENI HUDUMA ZA MATIBABU


Sehemu ya wakazi wa vijiji vya Masengwa, Ilobashi na Bubale ambao ni wazee waliohudhuria maadhimisho ya siku ya wazee duniani yaliyoadhimishwa kiwilaya katika kata ya Masengwa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, wakiwa wameonyesha bango lenye ujumbe unaoeleza haki wanazotakiwa kupata

Na Damian Masyenene –Shinyanga
KATIKA kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee nchini kwa kuwajali na kuwatunza, Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga mkoani hapa, imetoa vyeti (kadi) 5,568 za matibabu bure kwa wazee sawa na asilimia 43.1, huku vitambulisho vipya 7,859 vikiendelea kutengenezwa kwa ajili ya kundi hilo maalum ili kuliondolea usumbufu wanapokwenda kupata huduma za matibabu.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa Baraza la Wazee Wilaya ya Shinyanga, Boniface Boaz katika risala ya baraza hilo iliyosomwa kwenye maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyoadhimishwa kiwilaya katika kitongoji cha Kiloleni Kijiji na Kata ya Masengwa wilayani Shinyanga yakibebwa na kaulimbiu ya ‘Familia na Jamii tuwajibike kuwatunza Wazee’.

Ambapo alisema kuwa wilaya hiyo inao jumla ya wazee 13,176 wakiwemo wanaume 6,283 na wanawake 6,893, huku kukiwa kumeanzishwa mabaraza ya wazee katika kata zote 26 za halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na kuunganishwa kwenye mfumo wa wizara.

Akiwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee wa wilaya hiyo, Boaz alitaja kuwa wanahitaji huduma ya maji safi na barabara zinazopitika wakati wote, kupunguziwa bei ya nishati ya umeme, kuthaminiwa kwa kuwekewa ulinzi, kupatiwa mikopo katika halmashauri inayotokana na makusanyo ya ndani, kupewa pensheni kila mwezi kupata fedha za kujikimu na kupatiwa vitambulisho vya matibabu bure.

Kwa upande wake, Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo, Katibu Tawala Wilaya ya Shinyanga, Boniphace Chambi aliyemwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo, Jasinta Mboneko, alisema kuwa matukio ya mauaji ya wazee yanayotokea nchini hususan katika jamii ya Wasukuma, uchunguzi ulibaini kuwa familia na ndugu ndiyo wamekuwa wahusika, hivyo akatoa wito kwa wanajamii kuwajibika kuwatunza wazee na kubadili mawazo potofu kwamba uzee ni uchawi.

Chambi pia aliiagiza ofisi ya Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa wazee wote wanaoandikishwa na kupigwa picha kwa ajili ya kupewa kadi za matibabu bure basi wahakikishe wanakamilisha zoezi hilo na kuwapatia kwa wakati waanze matibabu ili kuondoa malalamiko ya nyuma ambapo walikuwa wanaandikishwa lakini hawapati kadi hizo.

“Tunashukuru kwa sasa matukio haya yamepungua, hivyo tuwajibike kuwatunza wazee wetu na tubadilishe mawazo kabisa na tuache hiyo kasumba kwa sababu uzee siyo uchawi bali ni Baraka. Tuiishi hii kaulimbiu na tujenge tabia ya kuwaenzi wazee tukiwa bado vijana,” alisema.

Akizungumzia matunzo ya wazee, Mratibu Shirika la TAWLAE linalojihusisha na kutetea haki za wazee mkoani Shinyanga, Eliasenya Nnko alisema changamoto kubwa ni kutoshirikishwa kwa kundi hilo katika vyombo vya utoaji maamuzi, kutokupata mikopo licha ya uwezo wao wa kipato na uzalishaji mali kupungua, ambapo alishauri kutiliwa mkazo kutungiwa sheria kwa Sera ya wazee ya mwaka 2003.

“Maadhimisho ya mwaka huu kwa wilaya yetu ya Shinyanga yamepata mwitikio mkubwa kutoka makundi yote kwenye jamii, kwa sasa hatuwazii sana kuwatenga wazee na familia kwa sababu kuwaweka kwenye vituo ni kuzidi kuwatenganisha na familia na kuwafanya wakose upendo, muhimu hapa ni jamii kuwajali na kuwatunza,” alisema.

Hata hivyo, takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto za mwaka 2020 zinaeleza kuwa tangu kuanza kutekelezwa kwa mkakati wa kitaifa wa kutokomeza mauaji dhidi ya Wazee uliozinduliwa mwaka 2014, mauaji ya wazee imepungua kutoka 557 mwaka hadi 74 mwaka 2019, ambapo hadi mwaka huu idadi ya wanaouliwa kwa sababu mbalimbali ni chini ya wazee 10 kwa mwaka.

Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo, Boniphace Chambi ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Shinyanga akizungumza kwenye sherehe hizo

Sehemu ya wageni mbalimbali wakiwemo watendaji wa Serikali katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wakifuatilia maadhimisho hayo
Mgeni rasmi, Boniphace Chambi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi waliohudhuria maadhimisho hayo ambao ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dk. Mameritha Basike (kulia) na Mratibu wa shirika la kutetea wazee (TAWLAE) Eliasenya Nnko (wa pili kutoka kushoto)



Katibu wa Baraza la Wazee wilaya ya Shinyanga, Boniface Boaz akizungumza na wananchi katika maadhimisho hayo

Mmoja wa wananchi wa Masengwa akielezea changamoto za wazee mbele ya mgeni rasmi kupitia ngonjera

Walinzi wa jeshi la Sungusungu walikuwa sehemu ya maadhimisho hayo, ambapo walitumbuiza wakiwa wamebeba ujumbe wa kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu

Wazee wakiendelea kupata huduma za vipimo vya magonjwa mbalimbali kwenye maadhimisho hayo

Wananchi na wazee wakishuhudia shughuli mbalimbali kwenye maadhimisho ya siku ya wazee duniani katika kata ya Masengwa





Akina mama wazee wakiwa wamebeba ujumbe unaohamasisha jamii na familia kuwalinda na kuwatunza wazee, wakati wa maadhimisho ya siku ya wazee duniani katika kata ya Masengwa wilayani Shinyanga.
Picha na Mpiga Picha wetu





























Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464