Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP, Debora Magiligimba akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Novemba 7,2020 akitoa taarifa kuhusu matukio mbalimbali yaliyojiri mkoani Shinyanga.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Umesikia kuhusu ile taarifa ya moto wa ajabu unaojiwasha na kuunguza magodoro,nguo na mito ya makochi ya watu Mjini Kahama??.... Sasa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wanafanya uchunguzi kuhusu tukio hilo katika kitongoji cha Hongwa mtaa wa Shunu Mjini Kahama ambalo limezua gumzo.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema ,moto huo wa ajabu unaohusishwa na imani za kishirikina umekuwa ukiunguza vitu vya ndani ya nyumba pekee kwenye nyumba ambazo hazina umeme tena nyakati za mchana tu.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo, Novemba 7,2020 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na jeshi la Zimamoto na Uokoaji wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo la moto kutokea na kuharibu mali nyumbani kwa Joseph Kioja Dida na majirani zake 8 katika mtaa wa Shunu Mjini Kahama.
Akisimulia kuhusu tukio hilo, Kamanda Magiligimba amesema mnamo Novemba 4,2020 majira ya saa mbili kamili usiku Joseph Kioja Dida (34) dereva pikipiki ‘bodaboda’ mkazi wa mtaa wa Shunu Mjini Kahama alifika kituo cha Polisi Kahama na kutoa taarifa kwamba huko nyumbani kwake kwa nyakati tofauti kumekuwa na tukio la kutatanisha la moto.
“Joseph Kioja Dida alisema moto huo umetoa takribani mara 30 na kuharibu/kuunguza mali mbalimbali za nyumbani hasa magodoro,mito ya makochi,nguo na bidhaa za dukani analomiliki nyumbani kwake tangu mwezi Agosti 2019 hadi sasa.
Hata hivyo hakuwahi kuripoti polisi wala Zimamoto kutokana na sababu za mazingira na namna moto huo unavyotokea bila kuwashwa na mtu yeyote akiamini kwamba moto huo unatokana na imani za kishirikina mpaka tarehe 04.11.2020 alivyoenda kutoa taarifa kituo cha polisi Kahama”,anasimulia Kamanda Magiligimba.
Kamanda huyo amesema, Kutokana na moto huo, Joseph Kioja Dida amepata hasara ya vitu mbalimbali kuungua na kuharibika vinavyokadiriwa kuwa na thamani ya jumla ya shilingi Milioni 2.
“Inasadikiwa kila mtu aliyenunua bidhaa kutoka dukani kwake mara baada ya kufika nyumbani moto huo hutokea na kuunguza bidhaa hizo. Hali hiyo imesababisha wapangaji kuhama kutoka kwenye nyumba yake kwenda kupanga sehemu zingine na watu wengine kuacha kununua bidhaa kutoka dukani kwake”,amesema Kamanda Magiligimba.
“Hata hivyo pamoja na wapangaji hao kuhama,moto huo umeendelea kutokea nyumbani kwa majirani na kuunguza vitu mbalimbali yakiwemo Magodoro,nguo za watoto,mito ya makochi”,ameongeza.
Amewataja majirani walioathirika na moto huo kuwa ni Adam Jackson ambapo moto huo uliunguza godoro lenye thamani ya shilingi 150,000/=, Anna Kachwele godoro na nguo za watoto zenye thamani ya shilingi 180,000/=, Benadetha John godoro,mito ya makochi na vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi Milioni Moja na Emmanuel Bundala, magodoro matatu na nguo za watoto zenye thamani ya shilingi milioni 1 na laki 5.
Wengine ni Saji Swalehe,godoro na nguo vyenye thamani ya shilingi 180,000/=, Joseph Masoud,godoro lenye thamani ya shilingi 80,000/= na Betri la Solar lenye thamani ya shilingi 50,000=, Teresia Nesphory,godoro na mito vyenye thamani ya shilingi 250,000/= na Laurent Charles, godoro lenye thamani ya shilingi 80,000/=.
Kamanda Magiligimba amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa matukio hayo ya moto huo hutokea wakati wa mchana na nyumba hizo hazina umeme.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464