AJIRA MPYA ZA WALIMU: SHULE ZA VIJIJINI NA WENYE ULEMAVU ZAPEWA KIPAUMBELE, KUANZA KURIPOTI DESEMBA 1 HADI 14 NA WATAKAOCHELEWA SIKU 14 AJIRA KUFUTWA


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Mhandisi Joseph Nyamhanga

Na Shinyanga Press Club Blog
LEO Novemba 27, 2020 Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Mhandisi Joseph Nyamhanga ametangaza orodha ya majina ya walimu waliopangwa kwenye vituo vya kazi Novemba 2020, yakijumuisha Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari pamoja na Mafundi Sanifu wa Maabara za Shule.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari ambayo imetolewa leo na Mhandisi Nyamhanga, ajira hizo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli alilolitoa Septemba 7, mwaka huu ambapo alitoa kibali cha ajira mpya za Walimu 13,000 wa Shule za Msingi na Sekondari pamoja na Mafundi Sanifu wa Maabara za Shule. 

"Nachukua fursa hii kuwafahamisha kwamba taratibu za ajira tajwa kwa awamu ya kwanza zimekamilika ambapo Walimu waliokidhi vigezo wamepangiwa vituo vya kazi. Serikali imeweka kipaumbele kuajiri walimu kwa ajili ya Shule za Sekondari zenye michepuo ya Sayansi na Hisabari, Ufundi, Kilimo na Biashara, Maarifa ya Nyumbani (Home Economics), Lugha ya Kiingereza, Lugha ya Kichina na Lugha ya Kifaransa. 

"Aidha, walimu wa masomo mengine wamepangwa katika vituo kulingana na upungufu uliopo ambapo kipaumbele ni Shule ambazo hazina kabisa walimu wa masomo husika. Kwa upande wa Shule za Msingi, upangaji wa walimu umefanyika kwa lengo la kuboresha uwiano wa walimu kwa wanafunzi," amesema.

Kwa muktadha huo, Ofisi ya Rais -TAMISEMI imewapanga zaidi walimu wa Shule za Msingi katika shule za vijijini ambako ndiko kwenye upungufu mkubwa zaidi wa walimu. Aidha, katika ajira hizi mpya walimu wenye ulemavu wamepewa kipaumbele. 

"Walimu waajiriwa wapya waliopangiwa vituo wanatakiwa kuripoti katika Ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri zinazosimamia shule walizopangiwa na baadaye kwenye shule husika. Walimu hao wanatakiwa kuripoti katika Halmashauri walizopangiwa kuanzia tarehe 01, Desemba 2020 hadi 14, Desemba 2020," amesisitiza.

Waajiriwa wapya ambao hawataripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya siku 14 kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 14 Desemba, 2020 watakuwa wamepoteza nafasi zao na nafasi zao zitajazwa na waombaji wengine wenye sifa waliopo kwenye Kanzidata (Database) ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI. 

PATA HAPA CHINI ORODHA YA MAJINA YA WALIMU HAO WAPYA




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464