ALIYEKUWA MWENYEKITI HALMASHAURI SIHA KUPITIA CHADEMA, AJITOSA TENA KUPITIA CCM

Muonekano wa makao makuu ya wilaya ya Siha

ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, kati ya mwaka 2015 na 2018 akiwa na kofia ya CHADEMA, Frank Kisinani, ameomba tena kuchaguliwa kuwania kiti hicho kupitia na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kisinani mwenye nafasi kubwa ya kurejea katika kiti hicho kama atateuliwa na CCM, atachuana vikali na Madiwani wengine ambao ni Dancan Urassa (Karansi), Juma Jani (Sanya Juu) na Humphrey Kifumu (Nasai).

Jana, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Siha, Mwanaidi Mbisha, alisema mbali na nafasi hiyo, pia wamo madiwani wanne walioomba nafasi ya Makamu Mwenyekiti.

“Ni kweli mpaka tunafunga shughuli za kupokea fomu za walioomba kuteuliwa na chama, kugombea nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, ni madiwani wateule wanne pekee wanaotaka uenyekiti na wanne pia wanaotaka umakamu mwenyekiti.

‘Kazi iliyopo mbele yetu ni ngumu ya kuchuja majina ya wanaoomba, na kisha sisi kuyapeleka ngazi husika kwa maana ya mkoa. Tutakuja na majina au jina la mtu mwenye sifa stahiki na anayeweza kuisogeza halmashauri kwa mchakamchaka wa maendeleo na sio mtu wa kusukumwa,” alisema.

Aidha, walioomba kuchaguliwa kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni pamoja na Susan Kihundwa (Kashashi) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM, Wilayani hapa, Lwite Ndossi maarufu ‘Nsonuu’ Patrick Kimaro (Ngarenairobi) na Noel Mollel (Ormelili).

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, lina historia ndefu ambayo haitasahaulika, kwa kuwa kati ya mwaka 2015 hadi 2018 liliongozwa na madiwani wengi wa CHADEMA, lakini mwaka 2018 lilibadilika na kuongozwa na CCM baada ya madiwani kuihama CHADEMA.

Waliokuwa madiwani wa CHADEMA wakati huo, walikihama chama hicho na kujiunga na CCM, baada ya aliyekuwa Mbunge wa Siha kupitia upinzani, Dk. Godwin Mollel, kujiunga na CCM na kisha kuchaguliwa tena kuwa mbunge kwa tiketi ya chama hicho mwaka 2019.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464