DAWA ZA KULEVYA KILOGRAM 119.074 ZA HEROIN, KILOGRAM 3.932 ZA COCAINE NA KILOGRAM 120 ZA BANGI ZATEKETEZWA JIJINI DSM KUFUATIA KESI ZAKE KUMALIZIKA MAHAKAMANI

Dawa za kulevya zikiwemo Kilogram 119.074 za Heroin, Kilogram 3.932 za Cocaine na kilogram 120 za bangi zimeteketezwa Jijini DSM baada ya kesi zake kumalizika mahakamani.

Zoezi la kuteketeza   dawa za kulevya  limefanyika jana jijini  DSM katika kiwanda cha Twiga Cement kilichopo Wazo Tegeta, limeshuhudiwa na Jaji wa Mahakama Kuu Edwin Kakolaki Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Biswalo Mganga, wawakilishi mbalimbali kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) akiwemo Kamishna ukaguzi na Sayansi jinai wa mamlaka hiyo Bertha Mamuya .

Akizungumza wakati wa zoezi la kuteketezwa kwa dawa hizo, Jaji Kakolaki amesema wanaziteketeza kwa sababu kesi zake zimekwisha malizika mahakamani.

“Kwa utaratibu uliopo, baada ya kesi za dawa za kulevya kuletwa mahakamani na tukapokea kielelezo cha dawa hizo, kesi ikimalizika mahakama utoa amri ya kuziteketeza na ndicho kilichofanyika leo hapa” Jaji Kakolaki

“Kimsingi hawa niliyowataja ni lazima wawepo kushuhudia amri ya mahakama ya uteketezaji wa vielelezo hivyo imefanyika tena kwa uwazi kabisa ili Watanzania waweze kujua kesi ikiisha lazima ziteketezwe na hii inajidhihirisha kuwa maneno ya mtaani kuhusu kwamba dawa hazifanyiwi chochote siyo ya kweli,” Jaji Kakolaki

Naye DPP, Mganga amesema “Dawa hizo zilizoteketezwa zimetokana na kesi 15 ambapo mwaka jana mwezi Oktoba tuliteketeza Kilogram 10.65 za cocaine na Kilogram 226.149 za Heroin ambazo zilitokana na kesi 17"

“Jumla ya kesi hizo yaani za mwaka jana na leo ni kesi 32 na jumla ya dawa za heroin tulizoteketeza kwa kipindi cha miaka miwili ni Kilogram 345.22 na Cocaine Kilogram 14.58 huku bangi ikiwa kilogram 120, hizo dawa za kulevya ni kwa mkoa wa DSM peke yake” DPP Mganga

“Hata hivyo sasa hivi tuliacha kusema dawa hizi zinathamani ya shilingi ngapi maana tuliona tunatoa motisha au kuhamamisha watu kwenda kufanya biashara hiyo, hivyo atuwezi kusema zina thamani kiasi gani bali tunasema zina madhara makubwa kwa binadamu,” Mganga   
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 


 





Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464