DOCTORS WITH AFRICA, FID Q WATEMBELEA VITUO VYA KUTOA HUDUMA ZA VVU NGOKOLO NA BUGISI, MRADI WAWAFIKIA WATU 293,000

Msanii Fid Q na mke wake wakiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa CUAMM na baadhi ya watoa huduma ngazi ya wanaofanya kazi kwa ushirikiano na Shirika la Doctors with Africa, leo nje ya jengo la ofisi ya shirika hilo iliopo eneo la Ngokolo Manispaa ya Shinyanga baada ya msanii huyo kutembelea ili kuona shughuli mbalimbali zinazotekelezwa.

Na Damian Masyenene, Shinyanga 
KUELEKEA Maadhimisho ya siku ya Ukimwii duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Desemba Mosi, Shirika la Doctrors with Africa yaadhimisha kwa kutembelea vituo vya tiba na matunzo katika Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga na Bugusi kata ya Didia Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga. 

Shirika la Doctors with Africa (CUAMM) linalojihusisha na Mradi wa Test & Treat (upimaji na matibabu) limefanya matembezi hayo leo Novemba 29, 2020 kwa kushirikiana na Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya wenye mahadhi ya HipHop, Fareed Kubanda maarufu kama FID Q aliyeambatana na mke wake. 

Walianza matembezi hayo katika kituo cha afya Ngokolo, ambapo Msanii Fid Q alikutana na wahudumu wa afya ngazi ya jamii hususan wanaohusika na mradi wa upimaji, matibabu na ufuatiliaji wa watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, pamoja na kujionea huduma mbalimbali zinazotekelezwa katika mradi huo wa test and treat. 

Akizungumza na wahudumu hao katika ofisi za Doctors With Africa (CUAMM) zilizopo katika kituo cha Afya Ngokolo, Fid Q aliwapongeza wahudumu hao kwa jitihada za kuwasaidia watu wanaoishi na VVU wajisikie huru, rafiki na hiari ya kupata matibabu pamoja na kuwarahisishia wahusika kupata dawa za kufubaza makali ya VVU kwa njia nyepesi. 

Ambapo, Fid Q na Mkewe walivutiwa na kazi kubwa inayofanywa na wahudumu hao kwa kushirikiana na Doctors with Africa, huku mama huyo ambaye anajihusisha na kutoa misaada katika shule akiahidi kusaidia chochote ili kuunga mkono jambo linalofanywa na Doctors With Africa katika kuwafikia watu wanaoishi na VVU. 

Akiwa katika Kituo cha afya Bugisi kilichopo Kata ya Didia halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, jopo la wafanyakazi wa Doctors with Africa pamoja na Fid Q walikagua shughuli mbalimbali zinazofanywa ikiwemo huduma ya upimaji na matibabu kwa watu wanaoishi na VVU, ambapo ameahidi kugharamia bima ya afya ya mmoja wa watoto waliozaliwa jana na kupewa jina la Fid Q. 

Jopo Hilo lilipokelewa na wanafunzi wa shule ya Msingi OLA Pre & Primary English Medium pamoja na watumishi wa kituo hicho cha afya wakiongozwa na Sister Kate ambaye aliwaongoza kukagua maeneo mbalimbali, huku akieleza kuwa wana jamii, watumishi pamoja na wanafunzi hawakuamini walipoelezwa kuwa watatembelewa na Msanii huyo mkubwa wa Hiphop nchini, hivyo akashukuru kwa ujio huo ambao umeleta matumaini na chachu kwa watoa huduma ngazi ya jamii kufanya kazi kwa ufanisi. 

Matembezi hayo yaliambatana na burudani mbalimbali za maigizo, nyimbo, ushuhuda wa baadhi ya wananchi wanaoishi na VVU pamoja na ushauri kutoka kwa wahudumu hao. 

Msanii Fid Q amesema mapokezi aliyoyapata na jitihada kubwa na kazi nzuri zinazofanywa na wahudumu hao ngazi ya jamii katika maeneo ambayo hayafikiki mara kwa mara ni jambo la kupongeza ambalo linapaswa kuigwa na watu wengine 

Akitoa taarifa ya mradi wa Test and Treat, Mratibu wa shughuli za Kijamii Shirika la Doctors with Africa (CUAMM), Gasaya Msira amesema mradi umekuwa na mafanikio makubwa kwani huduma imewafikia wananchi walio wengi tena kwa kuwafuata walipo na kwa mda wautakao. 

Amebainisha kuwa hadi kufikia Septemba, 2020 watu takribani 293,000 wamepata huduma ya upimaji kupitia mradi wa Test and Treat, vile vile takribani wateja 4,600 wameunganishwa na vituo vya tiba na matunzo, ambapo Gasaya amesema kuwa matarajio yao kuona jamii ikiendelea kuhamasika kupima afya zao ili kujua hali zao mapema ili kusaidia kutimiza malengo ya Milenia ya 95 95 95. 
Fid Q (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mratibu wa Shughuli za kijamii, Gasaya Msira juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa kwenye mradi wa Test and Treat unaotekelezwa na Shirika la Doctors with Africa, alipotembelea ofisi hiyo leo eneo la Ngokolo
Mmoja wa watoa huduma za afya katika kituo cha Ngokolo akitoa maelezo mbalimbali kwa msanii Fid Q na mkewe walipotembelea kituoni hapo
Mratibu wa shughuli za kijamii kutoka CUAMM, Gasaya Msira (kushoto) akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali kwa msanii Fid Q na mke wake walipotembelea ofisi za shirika hilo
Fid Q akijadiliana mambo mbalimbali na maafisa pamoja na watoa huduma za afya ngazi ya jamii nje ya jengo la ofisi za Shirika la Doctors with Africa lililopo Ngokolo muda mchache baada ya kutembelea ofisi hizo
Mmoja ya watoa huduma za afya ngazi za jamii wanaofanya kazi na shirika la Doctors with Africa (CUAMM) akifafanua namna wanavyowafikia watu wanaoishi na VVU
Msanii Fid Q akibadilishana mawazo na maofisa hao pamoja na watoa huduma za afya ngazi ya jamii katika kituo cha afya Ngokolo
Mke wa Fid Q akishukuru na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na wahudumu hao kwa kushirikiana na shirika la Doctors with Africa, ambapo ameahidi kusaidia chochote ili kuendelea kuwafikia watu wengi zaidi
Fid Q akipokelewa na wanafunzi wa Shule ya OLA pre & Primary School katika kituo cha afya Bugisi Kata ya Didia halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, ambapo walimkabidhi cheti cha kutambulisha mchango wake
Akina mama waliojifungua watoto katika kituo cha afya Bugusi wakibadilishana mawazo na Msanii Fid Q baada ya kutembelea wodi lao na kuwapongeza
Fid Q akiwa amembeba mtoto mchanga aliyezaliwa jana katika kituo cha afya Bugusi. Mtoto huyo alipewa jina la Fid Q, ambapo msanii huyo ameahidi kugharamikia bima yake ya afya.
Msanii Fid Q akifurahia baada ya kumbeba mtoto aliyepewa jina lake
Mtaalam wa Maabara katika kituo cha afya Bugusi, Dk. Elias Daud akitoa maelezo kwa msanii Fid Q namna wanavyofanya vipimo mbalimbali kituoni hapo
Dk. Elias akiendelea kutoa ufafanuzi kwa msanii Fid Q
Fid Q akiendelea kukagua shughuli mbalimbali katika kituo cha afya Bugusi
Fid Q akizungumza na wanafunzi, wafanyakazi wa kituo cha afya, wazazi na watoa huduma za afya ngazi ya jamii juu ya umuhimu wa kuendelea kuhamasisha upimaji na kuanza matibabu

Mmoja wa watoa huduma za afya ngazi ya jamii kutoka kata ya Tinde, Raphael Kamuli akitoa neno kwa niaba ya wenzake leo katika kituo cha afya Bugusi

Wanafunzi wakionyesha umahiri wa mazoezi ya viungo

Msanii FID Q (wa pili kushoto) akizungumza na baadhi ya watoa huduma ngazi ya jamii kutoka mitaa mbalimba katika kata ya Didia



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464