KAMATI YAREJESHA MALI ZA SH. BILIONI 3.3 ZILIZOPORWA SHIRECU, WALIOHUSIKA WAKALIA KUTI KAVU

Mwenyekiti wa timu iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa kufuatilia mali za chama kikuu cha ushirika Mkoani Shinyanga (SHIRECU), Asangye Bangu (kulia), akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, hati Saba za viwanja, nyumba na ghara ambazo ni mali za SHIRECU zilizokuwa zimeporwa na kuuzwa kinyume na taratibu (Picha na Marco Maduhu).

Na Damian Masyenene, Shinyanga 
TIMU Maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kwa ajili ya kufuatilia mali za vyama vya Ushirika vya Mwanza (NCU), Shinyanga (SHIRECU) na Kilimanjaro (KNCU), leo Novemba 23, 2020 imekabidhi mali zenye thamani ya Sh Bilioni 3.3 za Chama Kikuu cha Ushirika mkoa wa Shinyanga (SHIRECU) zilizokuwa zimeporwa na watu wachache isivyo halali. 

Makabidhiano hayo yamefanyika katika ukumbi wa jengo la Mkuu wa Mkoa mjini Shinyanga likishuhudiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya, Mrajisi Mkuu wa vyama vya ushirika, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, Wakuu wa Wilaya za Shinyanga na Kishapu pamoja na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Shinyanga na menejimenti ya Shirecu. 

Mali zilizokabidhiwa ni hati saba za viwanja kikiwemo kile kilichobainika kumilikiwa na mtoto mwenye umri wa miaka 15, ambapo zoezi la ufuatiliaji wa mali hizo lilifanywa kwa kupitia nyaraka za chama hicho na kuhoji watu ambao walikuwa wameuziwa wakiwamo watumishi wa Serikali na watu binafsi, na kufanikiwa kukomboa viwanja hivyo saba, ghara, pamoja na nyumba, huku wakiendelea kufuatilia mali zingine.  

Mwenyekiti wa timu iliyoundwa kufuatilia mali hizo, Asangye Bangu amesema viwanja sita vilivyoko eneo la Ushirika manispaa ya Shinyanga vilikuwa vimeporwa na baadhi ya watumishi wa manispaa ambao walicheza na mchoro wa ramani kasha kujigawia viwanja hivyo na baadae wakaviuza, hata hivyo baada ya ufuatiliaji wa timu hiyo baadhi ya wamiliki wa viwanja vitatu waliouziwa walikubali kutoa viwanja mbadala katika eneo la Ibadakuli na Ndala. 

Viwanja vingine viwili ambavyo vilikuwa havijaendelezwa, makubaliano yalifikiwa kwamba virudishwe SHIRECU na tayari zoezi hilo limekamilika, vilevile kati ya mali ambazo tayari zimerejeshwa ni jingo la ghorofa tatu lililopo Ilala Jijiji Dar es Salaam lenye wapangaji, pamoja na ghala la mizigo (Godown) lililopo neo la bandari Kurasini Temeke, Dar es Salaam lenye thamani ya Sh Bilioni 3 ambalo umiliki wake umerudishwa Shirecu. 

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya amesema kazi ya urejeshaji mali za vyama vya ushirika ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli alilolitoa Agosti 11, 2016, ambapo mbali na SHIRECU, tayari wamekabidhi mali 37 zenye thamani ya Sh Bilioni 61 kwa Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza (NCU). 

Kusaya ameeleza kuwa zoezi hilo ni endelevu kwani wanaamini kuwa mali nyingi za ushirika bado ziko mikononi mwa watu wanaozimiliki isivyo halali na kila kukicha wanagundua mali mpya. 

“Na mimi kama mtendaji mkuu wa wizara nitahakikisha mali zote zinarejeshwa, pia nitoe angalizo kwa Mrajis ahakikishe kupitia watendaji wake kuwa mali hizo zinazorejeshwa zitunzwe vizuri na ziendeshwe kwa wazi na kibiashara zaidi,” amebainisha. 

Kwa upande wake akipokea hati saba za mali zilizorejeshwa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack ameipongeza timu hiyo kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa umakini mkubwa, huku akiwataka watumishi wa SHIRECU kuzitambua mali zao zote kokote zilipo, kuvitembelea viwanja na kuviwekea alama ili visipotee na kuvamiwa na watu. 

“Nilipokea mali za Dar es Salaam kwa niaba ya Shirecu mfano ghorofa la Temeke, kwahiyo ushirika huu una mali za kutosha siyo maskini bali inahitaji wataalam kwasababu hapo ilipo haikopesheki inadaiwa Sh Bilioni 15…….katika hatua hizi pia twende zaidi tuone nani alisababisha hizi hasara na kama ni hatua zichukuliwe kwakuwa baadhi yao wapo, kwahiyo sheria ichukue mkondo wake,” amesema. 

Mwenyekiti wa SHIRECU, Lenis Jishanga ameishukuru wizara kwa hatua inazochukua ili kuubadilisha ushirika huo uweze kupiga hatua, huku akiahidi kuzisimamia mali zote za Shirecu kikamilifu na kuiomba menejimenti ya bodi ya chama hicho kubadilika na kuwa wabunifu.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (katikati), akimkabidhi Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya (Kulia), hati Saba za viwanja, nyumba na ghala ambazo ni mali za Chama Kikuu cha Ushirika Shinyanga (SHIRECU), Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya akizungumza wakati wa zoezi la kukabidhi hati saba za mali za Chama cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU).

 Mwenyekiti wa timu iliyoundwa na Waziri Mkuu kufuatilia mali za SHIRECU, Asangye Bangu akitoa taarifa namna walivyofanikiwa kukomboa mali za chama hicho, likiwamo Ghorofa lililopo Ilala Jijini Dar es salaam.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack (Kulia), akizungumza kwenye makabidhiano ya mali za SHIRECU.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Shinyanga (SHIRECU), Lenis Jishanga, akishukuru kupata mali hizo na kuahidi kuzitunza. 

Katibu mkuu wizara ya kilimo Gerald Kusaya, meza kuu akimkabidhi Mwenyekiti wa (SHIRECU) Lenis Jishanga, Hati saba za viwanja, nyumba na ghara, ambazo ni mali tena za chama hicho, wakwanza kushoto ni mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, kushoto, akishikana mkono na mwenyekiti wa SHIRECU Mkoa wa Shinyanga Lenis Jishanga, mara baada ya kukabidhiwa mali za SIHRECU, ambazo ziliuzwa kinyume na utaratibu.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (kulia), akishikana mkono na mwenyekiti wa SHIRECU, Lenis Jishanga, mara baada ya kukabidhiwa mali za ushirika huo ambazo ziliuzwa kinyume na utaratibu

Wajumbe wakiwa kwenye makabidhiano ya mali za chama kikuu cha ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU), ambazo ziliuzwa kinyume na utaratibu.
Wajumbe wakiwa kwenye makabidhiano ya mali za chama kikuu cha ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU), ambazo ziliuzwa kinyume na utaratibu.
Wajumbe wakiwa kwenye makabidhiano ya mali za chama kikuu cha ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU), ambazo ziliuzwa kinyume na utaratibu.
Wajumbe wakiwa kwenye makabidhiano ya mali za chama kikuu cha ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU), ambazo ziliuzwa kinyume na utaratibu.
Wajumbe wakiwa kwenye makabidhiano ya mali za chama kikuu cha ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU), ambazo ziliuzwa kinyume na utaratibu.
Wajumbe wakiwa kwenye makabidhiano ya mali za chama kikuu cha ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU), ambazo ziliuzwa kinyume na utaratibu.


Picha ya pamoja na ikipigwa mara baada ya kumaliza zoezi la kukabidhi mali za chama kikuu cha ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU).
Picha zote na Marco Maduhu

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464