MAKALA: SIRI YA UDHIBITI MAGONJWA YA MLIPUKO SHINYANGA YATAJWA, TAHADHARI YATOLEWA


Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Yudas Ndungile

Na Damian Masyenene -Shinyanga
KATIKA kuelekea msimu wa Mvua za mwisho wa mwaka na mavuno ya maembe, Mkoa wa Shinyanga umeeleza kuwa imara na tayari kwa tahadhari mbalimbali ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu, huku ikielezwa kwamba mkoa huo umefanikiwa kudhibiti ugonjwa huo kwa miaka mitano sasa tangu Septemba, 2016 aliporipotiwa mgonjwa wa mwisho wa kipindupindu.

Moja ya mikakati iliyowekwa na inayotekelezwa kwa muda na kupelekea mafanikio hayo ni kampeni ya ujenzi wa vyoo katika halmashauri zote sita, elimu ya usafi wa mazingira pamoja na upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kutoka Ziwa Viktoria.

MGANGA MKUU
Akizungumza na Shinyanga Press Club Blog, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Yudas Ndungile amesema kuwa wameanza mikakati mapema ya utoaji elimu ya usafi wa mazingira na kuhamasisha unawaji mikono kwenye taasisi za elimu (shule), watoaji huduma za fya ngazi ya jamii, wanaotoa huduma ya chakula (mama ntilie), vyoo vya umma, taasisi kubwa, kuosha matunda na uandaaji salama wa chakula.

Dk. Ndungile amesema kuwa kwa sasa mkoa huo hauna mgonjwa wa Kipindupindu na magonjwa mengine ya mlipuko, ambapo amesema halmashauri zinapaswa kuendelea kutekeleza mikakati iliyowekwa na kuendelea kutoa elimu kuelekea kipindi hiki cha masika na msimu wa maembe kuhusu kuosha matunda, kuweka vyombo vya kutupa taka, uandaaji salama wa vyakula na kunawa mikono.

“Tunayo pia kampeni ya matumizi bora ya choo kwa kuhamasisha ujenzi wa vyoo vya kisasa na kuvitumia, pia tunasisitiza kwamba choo siyo kwa ajili ya kumuonyesha afisa afya bali ni kwa matumizi yako…..lengo ni kutokuwa kabisa na tatizo la magonjwa ya mlipuko.

“Tunatoa wito sasa kwa wamiliki wa taasisi kubwa, migahawa, baa, sehemu za chakula na kumbi za starehe watu wanawe mikono kwa vitakasa mikono, waoshe matunda na wasafishe vyoo, utupaji wa taka watu wafuate kanuni kwa kuweka ndoo ama mifuko nyumbani ili kuepusha inzi kuzaliana kwa wingi” amesisitiza Dk. Ndungile.

AFISA AFYA
Akizungumzia kampeni ya matumizi ya vyoo, Afisa Afya wa Mkoa wa Shinyanga, Neema Simba amesema kuwa tangu kuanza kwa mradi huo mwaka 2014 katika mkoa huo, kwa mujibu wa takwimu za Aprili hadi Juni, 2020, matumizi ya vyoo bora ni asilimia 60, huku asilimia 98 ya watu wakiwa na uwezo wa kutumia huduma ya choo na asilimia mbili wakiwa hawana vyoo.

Ameongeza kwa kubainisha kuwa asilimia 32.38 ya watu wananawa maji safi na sabuni, kaya zenye vyoo vya asili (vya magunia, visivyo na milango) ikiwa ni asilimia 38, kaya zinazotunza vyoo vizuri (kusafisha vyoo na kuvitumia vizuri) ni asilimia 26.54, hivyo kuepuka magonjwa ya mlipuko ikiwemo Typhoid, U.T.I na magonjwa ya kuhara, ambapo malengo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ni kufikia asilimia 80 ya vyoo bora. 

Afisa Afya wa Mkoa wa Shinyanga, Neema Simba

Neema ameeleza kuwa kabla ya kuanza kwa kampeni hiyo mwaka 2014, mkoa wa Shinyanga ulikuwa na vyoo bora asilimia 17 tu, ambapo elimu kwenye kaya ilisaidia kuwabadilisha wana jamii hususani maeneo ya vijijini, ambapo ilibidi kuitisha vikao na kukusanya vinyesi vichakani kisha kuletwa mkutanoni na kuelezewa madhara na kwanini wanapaswa kuwa na vyoo, ndipo wanajamii wakabadilika na kuwekeana maazimio ya kuwa na vyoo na kutoa faini kwa wasiojenga vyoo.

“Kuwa na vyoo kumesaidia kwa namna nyingine kuondoa dhana potofu ya kwamba watu kufariki kwa magonjwa hayo yatokanayo na uchafu eti wanarogwa, watu walikuwa wanaugua vitu ambavyo wanajitakia na kutumia gharama kubwa kwenye matibabu, tunashukuru watu wa vijijini walielewa na kubadilika,” amefafanua.

MIKAKATI YAENDELEA
Akielezea mikakati zaidi kuhusu kampeni ya vyoo bora, Afisa Afya wa Mkoa wa Shinyanga, Neema Simba amesema kuwa kwa sasa wanajikita kwenye kuboresha vyoo ili jamii iwe na vyoo ambavyo shimo limejengewa chini ili kuwe na vyoo imara na vinavyoweza kusafishika na kuachana na vile vya asili.

“Baada ya watu kuelewa umuhimu wa kuwa na choo, sasa changamoto imebaki kuwa ni choo cha namna gani na kufanyiwa usafi kwa sababu watu wanajisaidia bila kufanya usafi, na tunasisitiza kwamba vyoo vya shule, stendi, ofisi kubwa, kanisani vinatakiwa visafishwe mara tatu kwa siku.

“Bado tunaendelea kugawa vifaa vya kunawia mikono na tunahamasisha sana unawaji mikono na usafi wa vyombo hasa ofisi zinazokutanisha watu wengi, kwenye migahawa na sehemu za chakula, usafi wa vyombo ni muhimu baada ya kuviosha vianikwe juani kuua bakteria na maji ya kunywa yachemshwe ama yawekewe dawa ya kuua bakteria,” alisema.

WANANCHI 
 Baadhi ya wakazi wa manispaa ya Shinyanga, akiwemo Yasinta Baraka, John Maduhu na Elizabeth Bundala wamesema kuwa wamechukua tahadhari zote kuelekea kipindi cha mvua kwa kufuata ushauri wanaopewa na wataalam wa afya ngazi za jamii ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.

Elizabeth Bundala ambaye anatoa huduma ya chakula mjini humo, amebainisha kuwa, amekuwa akitembelewa na wataalam wa afya mara kwa mara kupewa elimu na kwamba amekuwa akifuata ushauri huo, huku akiomba viongozi wa Manispaa kuahikikisha wanazoa/kubeba taka kwa wakati ili kuepusha wadudu kuzaliana.

“Sisi tunafuata maelekezo yote na tunatunza taka kwenye ndoo na mifuko, lakini changamoto kubwa ni uzoaji, taka zinaweza kumaliza miezi miwili gari la halmashauri halijaja, wakati sisi wapikaji tunazalisha taka nyingi kwahiyo inakubidi uingie gharama kwenda kuzitupa,” amesema.

Naye John Maduhu alilalamikia kitendo cha maghuba ya kuhifadhi taka (dampo) kukaa na uchafu kwa muda mrefu zaidi ya miezi mitano na kuleta kero kwa wananchi na kusababisha taka kutapakaa kwenye makzi ya watu na kuzalisha magonjwa, hivyo kuomba mamlaka kulifanyia kazi jambo hilo.

NEMC
Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) iliyotolewa Septemba 23, mwaka huu na Mkurugenzi wa baraza hilo, Dk. Samuel Gwamaka mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ilieleza kupungua kwa kasi ya magonjwa ya mlipuko hususani kipindupindu hapa nchini kutokana na usimamiaji mzuri wa sheria na kanuni za mazingira na utoaji wa elimu hasa katika kipindi cha awamu ya tano.

“Tumepata mafanikio makubwa kwani takwimu zinaonesha magonjwa ya milipuko kama kipindupindu kasi ya kuenea kwake imepungua sana, sikumbuki kama tumekumbana na kipundupindu miaka mitano iliyopita,’’ alisema.

Dk. Gwamaka aliongeza kwamba chanzo kikubwa cha magonjwa ya milipuko nchini ni utiririshaji wa maji taka katika maeneo ya makazi ya watu pamoja na maji ya kemikali zenye sumu kutoka viwandani ambayo huelekezwa katika mito na makazi ya watu.

HUDUMA YA MAJI SHINYANGA
Akitoa taarifa kwa viongozi kutoka Wizara ya Maji iliyotembelea miradi ya maji mkoani Shinyanga mnamo Oktoba 7, mwaka huu, Meneja wa Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Julieth Payovela alisema upatikanaji maji katika mkoa huo wenye wakazi zaidi ya Milioni 1 huku asilimia 79.5 ya wakazi wake wakiwa vijijini na 20.5 mjini, hadi Septemba, mwaka huu upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini ni asilimia 60.03 na mijini asilimia 70, na upatikanaji wa jumla wa maji safi na salama mkoani hapa ni asilimia 66.1 kupitia mamlaka tatu za KASHUWASA, SHUWASA na KUWASA.

MFUMO WA MAJITAKA NI TATIZO
Akieleza baadhi ya changamoto katika utoaji maji kwenye miji ya Kahama na Manispaa ya Shinyanga, Dk. Payovela alisema kuwa, mojawapo ya changamoto zinazowakabili katika kutoa huduma mkoani humo ni kukosekana kwa mfumo wa majitaka katika miji hiyo.

Hata hivyo, Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira mjini Shinyanga (SHUWASA), imeeleza kuwa kwa sasa mamlaka hiyo haina mfumo wa uondoaji majitaka na kupelekea huduma ya uondoaji majitaka kufanywa na Manispaa ya Shinyanga kupitia idara ya afya, huku ikielezwa kuwa, katika mpango wa maendeleo wa sekta ya maji (WSDP) awamu ya kwanza mtalaam muelekezi ambaye ni GIBB Afrika amekamilisha kazi ya kuandaa makablasha ya miundombinu hiyo na kuwasilisha wizara ya maji kwa hatua zaidi.

“Matarajio yaliyopo ni kwamba, katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa sekta ya maji awamu ya pili (WSDP II) na kama fedha itapatikana ujenzi wa mfumo wa uondoaji majitaka unaweza kutekelezwa,” ilieleza taarifa ya Shuwasa. 

 Mmoja wa akina mama wanaotoa hudumaya chakula (Mama Ntilie) akiandaa chakula kwa ajili ya wateja wake (Picha na Mtandao)





Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464