MBUNGE KATAMBI KUITAFUTIA STAND UNITED WAFADHILI WATAKAOIRUDISHA LIGI KUU

 Mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini, Patrobas Katambi, akizungumza na waandishi wa habari na kuelezea mikakati yake ya kuinyanyua kiuchumi mji wa Shinyanga na kufikia hadhi ya kuwa jiji, pamoja na kuinyanya tena timu ya Stand united kushiriki kucheza ligu kuu.

Na Marco Maduhu, Shinyanga 
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi (CCM), ameahidi kutafuta wafadhili ambao wataiwezesha kifedha timu ya Stand united ya mjini Shinyanga, ili kusajili wachezaji wazuri ambao watairudisha tena kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
 
Katambi amebainisha hayo leo Novemba 30, 2020 kwenye kikao chake na waandishi wa habari mjini Shinyanga, kuwa moja ya mikakati yake ya kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo na kuiinua timu ya Stand United ijikwamue iliko na kurudisha makali yake na hatimaye kucheza tena Ligi Kuu. 

Amesema timu hiyo inahitaji fedha kwa ajili ya kusajili wachezaji wazuri pamoja na kuwalipa mishahara kwa wakati, na kuahidi kutafuta wafadhili ambao wata iwezesha kifedha na hatimaye kuinuka tena na kushiriki kucheza ligi kuu. 

“Hapa sasa hivi nina mipira ambayo nitaikabidhi kwenye uongozi wa timu ya stand united kwa ajili ya kufanyia mazoezi, na nitawatafutia vifaa vingine vya mazoezi, na lengo langu ni kuhakikisha timu hii inarudi tena kushiriki kucheza ligi kuu,” amesema Katambi. 

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA), Stephen Mihambo, akizungumza na Shinyanga Press Club Blog kwa njia ya simu, amepongeza juhudi hizo ambazo anazionyesha Mbunge Katambi, za kutaka kuirudisha timu ya Stand united ligi kuu, na kubainisha kuwa mpira ni gharama na kuahidi kumpatia ushirikiano. 

Stand United maarufu kama Chama la Wana ama Wapiga debe wa Shinyanga, kwa mara ya mwisho ilishiriki michuano ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/19 na kushuka daraja hadi la kwanza ambapo nako ilishindwa kufurukuta na kujikuta daraja la pili inakohaha kujinasua.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464