MKURUGENZI MSAIDIZI WA ELIMU TAMISEMI AKAGUA UJENZI SEKONDARI YA MWADUI TECH.

Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu Sekondari kutoka TAMISEMI, Benjamin Oganga akikagua moja ya majengo yanayokarabatiwa kwenye mradi huo katika shule ya Sekondari Mwadui Technical.

Na Shinyanga Press Club Blog
Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu Sekondari kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI, Benjamin N. Oganga ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa na mabweni katika Shule ya Sekondari Mwadui Technical iliyopo Wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga.

Ujenzi wa majengo hayo unakarabati jumla ya Sh Milioni 346, unaojumuisha kiasi cha Sh 226,856,239.82 kutoka serikali kuu za ukarabati wa majengo, Sh Milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi na Sh Milioni 40 za ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa.

Mkurugenzi huyo alifanya ukaguzi huo jana Novemba 9, 2020 katika shule hiyo, ambapo ujenzi huo unahusisha ukarabati wa majengo, ujenzi wa mabweni na vyumba viwili vya madarasa ya shule hiyo. 

Shule hiyo iliyopo katika Wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga ilianzishwa mwaka 1997 chini ya Mgodi wa Almasi wa Williamson yenye jumla ya wanafunzi 827 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne huku wanafunzi wa kike wakiwa ni 437 na wakiume 390. 

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Oganga amepongeza maendeleo ya ujenzi huo, huku akiwataka kusimamia kwa umakini ujenzi huo ili majengo yawe imara na kushauri fedha zinazobaki zitumike kupaka rangi na kuweka bati mpya kwenye majengo mengine.

“Nataka mwenge ujao utakapopita hapa pawe mfano kwa maana ya ubora wa majengo. Pia fedha zitakazobaki kutokana na ujenzi huu zitumike kukupaka rangi majengo mengine ili yawe ya kufanana na haya yaliyorekebishwa," alisistiza.

Mkuu wa shule hiyo, Shija Dominic Kulewa ameishukuru serikali na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kwa kutenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo huku akiahidi kusimamia ukarabati na kukamilisha ujenzi huo.

“Nashukuru sana kwa ajili ya huu ukarabati kwani majengo ya shule hii yalikuwa yamechakaa sana, kutokana na nyufa zilizokuwepo katika madarasa ilikuwa inapelekea wanafunzi kukaa darasani kwa wasiwasi sana. Hivyo natoa pongezi za dhati kwa serikali yetu kwa kuipa elimu kipaumbele," alisema Kulewa.


Sehemu ya majengo yaliyojengwa kupitia mradi huo katika shule ya Sekondari Mwadui Tech

Mafundi wakiendelea na ujenzi katika moja ya majengo shuleni hapo


Picha na Catherine Ngowi

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464