NKULILA APITA BILA KUPINGWA UMEYA, JIJIMYA NA NGASSA NAO WAPETA WENYEVITI KISHAPU, SHY DC


 Mstahiki Meya Mteule wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (aliyevaa miwan) na madiwani wa manispaa hiyo leo baada ya kukamilika kwa zoezi la uchaguzi katika ofisi za CCM wilaya ya Shinyanga mjini.
 
Na Damian Masyenene- Shinyanga
MADIWANI wa Halmashauri za Wilaya ya Shinyanga na Kishapu wamefanya uchaguzi wa Wenyeviti na Makamu wa halmashauri hizo, huku wale wa Manispaa ya Shinyanga wakiwachagua Mstahiki Meya na Naibu wake, ambapo Diwani wa Kata ya Ndembezi, David Nkulila (CCM) amepita bila kupingwa katika nafasi ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga akipigiwa kura zote 23 za ndiyo.

Nkulila amechaguliwa leo Novemba 24, 2020 katika uchaguzi uliofanyika kwenye ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, huku Esther Festo Makune akishinda nafasi ya Naibu Meya kwa kupata kura 17 kati ya 23, akifuatiwa na Mariam Nyangaka wa Kata ya Kitangiri aliyepata kura nne na Ruben Kitinya wa Kata ya Kizumbi akipata kura mbili.

Katika Halamashauri ya Wilaya ya Shinyanga, aliyekuwa Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ngassa Mboje ametetea nafasi hiyo kwa ushindi wa kura 20 dhidi ya Amos Mshandete wa Kata ya Ilola aliyepata kura 16.
 
Isack Sengerema wa Kata ya Iselamagazi ameshinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kupata kura 19 dhidi ya Hamis Masanja wa kata ya Samuye aliyepata kura 17.
 
Kwa upande wa halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ambao walifanya uchaguzi jana Novemba 23, 2020, Diwani wa Kata ya Mondo, William Luhende Jijimya alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa halmashauri hiyo kwa kura 24, huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti ikienda kwa Anderson Mandiya wa Kata ya Ukeyenge aliyepata kura 15.
 
 
 Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Said Bwanga (kushoto) pamoja na baadhi ya madiwani wa manispaa ya Shinyanga waliohudhuria uchaguzi wa Mstahiki Meya wa manispaa hiyo leo katika ofisi za chama hicho.

Mstahiki Meya Mteule wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila (kushoto) akipongezwa na Diwani wa Kata ya Ngokolo, Victor Mkwizu baada ya kupita bila kupingwa katika uchaguzi uliofanyika leo mjini Shinyanga

  

Diwani wa Kata ya Kambarage, Ramadhan Mwendapole (kulia) akimpongeza Mstahiki Meya Mteule wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila baada ya kutangazwa mshindi leo akipita bila kupingwa

 

 Mstahiki Meya Mteule wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila (kushoto) akipongezwa na baadhi ya madiwani wa manispaa hiyo

 Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Esther Festo Makune (kulia) na Mstahiki Meya, David Nkulila (kushoto wakiwa katika picha ya Pamoja na Diwani wa Kata ya Kitangiri, Mariam Nyangaka (katikati) baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo, huku diwani huyo akiambulia nafasi ya pili kwenye kinyang'anyiro cha unaibu meya.

 

 



 Picha mbalimbali zikiwaonyesha Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila na Naibu wake, Esther Makune wakiwa katika picha za pamoja na baadhi ya madiwani baada ya kukamilika kwa zoezi la uchaguzi leo kwenye ofisi za CCM
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464