Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli akiwa bungeni leo
Na Shinyanga Press Club Blog
LEO Novemba 13, 2020 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli amelihutubia na kulifungua rasmi Bunge la 12, huku akiahidi kushughulikia mambo mbalimbali ikiwemo suala la maji jijini Dodoma na kuboresha vitambulisho vya Machinga.
Rais Magufuli amesema vitambulisho vya Machinga vitaboreshwa na moja ya maboresho hayo ni kuweka picha ya mhusika na kuwasaidia machinga kupata mikopo ya kuboresha biashara zao.
Pia Rais Magufuli ameweka wazi kuwa wabunge wanapaswa kukosoa mambo ambayo hayako sawa, huku akifafanua kuwa hawapaswi kukosoa ilimradi, bali wakosoe kwa hoja na kutoa mapendekezo ya kujenga.
Katika hatua nyingine, JPM ametoa wito kwa viongozi wa Serikali za Mkoa, Wilaya, Tarafa, Vijiji na Kata kote nchini kuweka utaratibu wa kutenga siku ya kuzungumza na wananchi na kusikiliza kero zao.
"Nategemea ushirikiano mkubwa kwa bunge hili, nasi serikali tunaahidi kutoa ushirikiano kwa bunge hili na mhimili wa mahakama ....Tukishirikiana vizuri na bunge hili, miaka mitano ijayo itakuwa ya maajabu, nataka niwahakikishie kwamba mimi niko pamoja na nyinyi na kamwe sitawaacha," amesema Rais Magufuli.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464