RAIS MWINYI ATANGAZA MAWAZIRI, AWAANDIKIA ACT WAZALENDO, AMTUMBUA MKURUGENZI WA AFYA



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametangaza baraza jipya la mawaziri leo Novemba 19, 2020, ambapo wizara mbili bado hajateua mawaziri (Wizara ya Afya na Wizara ya Biashara) akisema pia hajateua naibu waziri yeyote na kwamba atateua iwapo ataona kuna wizara inahitaji naibu.

Akizungumza wakati wa kutangaza baraza hilo, amesema: “Tumekutana leo katika shughuli muhimu ya kutangaza baraza la mawaziri, watu wamekuwa wakisubiri kwa hamu na kwamba imeonekana kama vile limechelewa lakini kwa mujibu wa katiba bado liko ndani ya muda unaotakiwa.

“Ofisi ya Rais badala ya kuwa na mawaziri watatu sasa itakuwa na mawaziri wanne, tutakuwa na Waziri wa Uchumi na Uwekezaji, Waziri wa Tawala za Mikoa na Idara Maalum, Waziri wa Katiba na Utawala Bora na wa 4 ni Waziri wa Nchi Fedha na Mipango.

“Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais kutakuwa na waziri mmoja atakayeshughulika na sera, uratibu na shughuli za baraza la wawakilishi, tuna wizara ya kilimo, umwagiliaji, maliasili na mifugo, tumeiondoa uvuvi tunataka kuipa mkazo wa peke yake,” amesema Mwinyi.

Aidha, Rais Mwinyi amemteua Jamal Kassim Ali mwenye umri wa miaka 36, kuwa Waziri wa Fedha, Bi. Tabia Mwita Maulid kuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Rais Mwinyi pia amesema amekiandikia barua ACT- Wazalendo kukiomba kupeleka jina la makamu wa kwanza wa rais baada ya chama kupata asilimia ya zaidi ya 10 kwa mujibu wa Katiba.

BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI ZANZIBAR:

1. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uchumi na Uwekezaji – Mheshimiwa Mudrik Ramadhan Soraga.

2. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) – Mheshimiwa Masoud Ali Mohammed.

3. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba na Utawala Bora – Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman.

4. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango – Mheshimiwa Jamal Kassim Ali.

5. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi – Mheshimiwa Dokta Khalid Mohammed Salum.

6. Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji na Mifugo – Mheshimiwa Soud Nahoda Hassan.

7. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali – Mheshimiwa Simai Mohammed Said

8. Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni – Mheshimiwa Tabia Mwita Maulid.

9. Wizara ya Biashara ya Maendeleo ya Viwanda. Hakuna Waziri.

10. Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi – Mheshimiwa Riziki Pembe Juma.

11. Wizara ya Maji na Nishati – Mheshimiwa Suleiman Masoud Makame.

12. Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto. Hakuna Waziri.

13. Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale – Mheshimiwa Lela Mohammed Mussa.

14. Wizara ya Uchumi wa Bluu na Uvuvi – Mheshimiwa Abdallah Hussein Kombo.

15. Wizara ya Ujenzi – Mheshimiwa Rahma Kassim Ali.
Rais Mwinyi Atengua Uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Afya


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Afya katika Wizara ya Afya, Dkt. Jamala Adam Taib kuanzia Novemba 18, 2020.

Aidha, Dkt. Mwinyi ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja, Dkt. Ali Salum Ali. Dkt. Mwinyi amefikia uamuzi huo baada ya kufanya ziara katika hospitali hiyo ili kujionea mwenyewe hali ya utoaji wa huduma na changamoto zinazoikabili hospitali hiyo. Kufuatia utenguzi huo, Dkt. Mwinyi amesema wote ambao uteuzi hao umetenguliwa watapangiwa kazi nyingine.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464